Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Mkoa wa Iringa unatekeleza vizuri mwongozo wa tuzo ya Rais ya utunzaji wa mazingira na uhifadhi ya vyanzo vya maji na Manispaa ya Iringa kushika nafasi ya kwanza kwa Manispaa zote nchini.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akisoma taarifa ya maendeleo ya Mkoa wa Iringa kwa makamu wa Rais mama Samia Suluhu Hassan aliye katika ziara ya siku tano mkoani Iringa jana.
Masenza alisema kuwa Mkoa wa Iringa ulipokea na kutekeleza mwongozo wa tuzo ya Rais ya utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya maji. “Katika mwaka 2015 Manispaa ya Iringa ilishika nafasi ya pili, mwaka 2016 ilishika nafasi ya kwanza kwa Manispaa zote Tanzania na mwaka 2017 ilishika nafasi ya tatu kwa Manispaa zote Tanzania” alisema Masenza.
Akiongelea zoezi la upandaji miti na uhifadhi wa mazingira, mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa Mkoa kwa kushirikiana na wadau wa maliasili umeweza kushiriki kikamilifu katika zoezi la upandaji miti na uhifadhi wa mazingira. Aliyataja mafanikio yaliyopatikana kuwa ni
Kuvuka lengo la upandaji miti 55,000,000 kwa msimu 2016/2017 na kupanda miti 56,108,532. Katika zoezi hilo miti 47,766,366 sawa na asilimia 86.84 ilipona. Juhudi nyingine alizitaja kuwa ni kufanya oparesheni maalum ya kubaini na kuondoa wavamizi na mifugo katika hifadhi ya jamii ya Mbomipa wilayani Iringa. Alisema kuwa oparesheni ilifanyika chini ya kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa ilikamata watuhumiwa 38 wakiwa na mifugo 2,067 na kesi 6 zilifunguliwa mahakamani.
“Halmashauri zote Mkoani Iringa zimetakiwa kuendelea kudhibiti maeneo yote ya hifadhi yasiingizwe mifugo na pia kuendelea kutambua na kupiga chapa mifugo katika maeneo ya Halmashauri ili kuweza kudhibiti mifugo inayoingia bila kufuata taratibu” alisema Masenza.
Kuhusu shindano la usafi wa mazingira lililohusisha halmashauri za majiji, miji na wilaya kwa mwaka 2014, katika ngazi ya Manispaa zote Tanzania, Manispaa ya Iringa ilishika nafasi ya kwanza kitaifa na wilaya ya Mufindi ilishika nafasi ya pili kitaifa wakati kijiji cha Ifunda kikishika nafasi ya kwanza kitaifa.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.