IRINGA WATAKIWA KUJIUNGA NA BIMA YA AFYA
Na. Dennis Gondwe, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa -IRINGA
Wananchi wa mkoa wa Iringa wametakiwa kujiunga na mfuko wa Taifa wa bima ya afya ili waweze kunufaika na matibabu bila malipo pindi wanapougua. Kauli hiyo iliyolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, mheshimiwa Amina Masenza alipokuwa akiongea katika kipindi moja kwa moja cha Nyota ya asubuhi kinachorushwa na kituo cha redio Furaha cha mjini Iringa leo.
Mheshimiwa Masenza alisema “ombi langu kwa wananchi wa mkoa wa Iringa, tuendelee kujiunga na mfuko wa bima ya afya ili tuendelee kutibiwa bila bugdha”. Alisema kuwa matibabu ni gharama kubwa ila kwa mwananchi aliyejiandaa vizuri, hawezi kupata tatizo la gharama ya matibabu pindi anapougua. Alisema kuwa bima ya afya ni mkombozi kwa wananchi wa kawaida ambao wanapougua hujikuta hawana fedha za kugharamia matibabu.
Aidha, alishauri wananchi hao kuwakatia bima watoto kwa gharma ya Tshs 54,000 ambayo itamuwezesha kutibiwa bure. Alisema kuwa bima ya watoto ni muhimu kwa sababu watoto wengi ni wahanga wa magonjwa kwa sababu kinga yao ya mwili haijaimarika vizuri. “Bima ya watoto kwa Tshs 54,000 itawawezesha watoto kutibiwa sehemu mbalimbali bila gharama” alisema mheshimiwa Masenza.
Akiongelea kampeni ya kupima afya “Afya check campaign” Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Dr Faith Kundy alisema kuwa Manispaa ya Iringa itakuwa mwenyeji wa kampeni ya kupima afya itakayozinduliwa kesho na mkuu wa mkoa wa Iringa, Mheshimiwa Amina Masenza katika uwanja wa bustani ya Manispaa (Garden) kwa lengo la kuwapatia fursa wananchi wa Manispaa kupima hali ya afya zao bure. Alisema kuwa katika kampeni hiyo magonjwa yasiyo ya kuambukiza na magonjwa ya kuambukiza yatapimwa bure. Kampeni ya kupima afya itakwenda sambamba na ugunduzi wa kifua kikuu ngazi ya jamii.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.