Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Kamati ya kitaifa ya ushauri wa misitu imetakiwa kukamilisha rasimu ya sera mpya ya Taifa ya misitu mapema na kumshauri waziri mwenye dhamana juu ya uendelevu wa rasilimali misitu nchini.
Agizo hilo lilitolewa na waziri wa maliasili na utalii Dr. Hamis Kigwangala alipokuwa akifungua kikao cha tatu cha kamati ya kitaifa ya ushauri wa misitu kilichofanyika katika ukumbi wa VETA mjini Iringa jana.
Dr. Kigwangala alisema kuwa kamati hiyo inawajibu wa kupitia rasimu na kushauri ipasavyo juu ya uendelevu wa rasilimali misitu. “Hata hivyo, lipo jukumu jingine muhimu sana ambalo bila hilo utendaji wetu katika sekta hii utakuwa mgumu sana. Jukumu hilo ni ukamilishwaji wa rasimu ya sera mpya ya Taifa ya misitu. Kamati hii inao wajibu wa kuipitia rasimu hii na kumshauri waziri kama inakidhi matarajio ya uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali hii au la. Hivyo, nimeridhia rasimu hii mpya kuletwa kwenu baada ya kukamilisha hatua za kukusanya maoni toka kwa wadau tofauti tofauti nchi nzima” alisema Dr. Kigwangala. Aidha, aliitaka kamati hiyo kutotumia muda mrefu kupitia rasimu hiyo na kutoa maoni yao. Alisema kuwa sera hiyo imechelewa sana na kuitaka kamati hiyo kulipa kipaombele suala la upitiaji wa sera hiyo.
Katika salamu za mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema kuwa wizara imekuwa ikiunga mkono juhudi za kuendeleza utalii kwa Mkoa wa Iringa na mikoa ya nyanda za juu kusini. “Pongezi kwa juhudi za wizara ya maliasili na utalii kuunga mkono juhudi za kuendeleza utalii mkoani Iringa” alisema Masenza. Aidha, alimhakikishia waziri wa maliasili na utalii kuwa Mkoa wa Iringa umejipata vizuri katika kukuza na kuendeleza utalii kwa ukanda wa kusini.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.