Serikali ya Mkoa wa Iringa imekiagiza kiwanda cha karatasi Mufindi (MPM) kuanza kuzalisha karatasi nyeupe ili kuongeza ajira kwa vijana na mapato ya Serikali.
Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe Ally Hapi alipokuwa akiongea na menejimenti ya kiwanda hicho baada ya kufanya ziara ya kukikagua jana.
Mhe Hapi alikiagiza kiwanda hicho kuanza kutengeneza karatasi nyeupe zinazotumika katika shajala mbalimbali kwenye ofisi na madaftari. Alisema kuwa wakati wa kukagua kiwanda hicho, amekuta mashine za kutengeneza karatasi nyeupe zimezimwa jambo linaloikosesha Serikali mapato. “Ndugu zangu, uzalishaji wa karatasi nyeupe katika kiwanda hiki utasaidia kuongeza ajira kwa vijana wetu, utapunguza gharama kubwa ya kununua karatasi nyeupe na kuongeza mapato ya Serikali. Hiki ni kiwanda kikubwa kilichokuwa kinategemewa na nchi.” alisema Mhe Hapi.
Mkuu wa Mkoa alisema kuwa eneo la kiwanda hicho lina uwekezaji mkubwa uliofanywa na Baba wa Taifa Mwl Julius Nyerere katika awamu ya kwanza ya utawala wake. “Serikali ya Mkoa inataka kubaini malengo ya Baba wa Taifa aliyokuwa nayo katika kiwanda hiki hadi mataifa mbalimbali yalikuwa yanakuja kujifunza katika kiwandani hapa. Nataka kujua masharti yaliyotolewa na Serikali wakati wa ubinafsishaji kama yametekelezwa na muwekezaji” alisema Mhe Hapi.
Vilevile, alishangazwa na reli ya TAZARA sehemu ya mchepuko wa kuingia kiwandani hapo kutokufanya kazi kwa muda mrefu. Alisema kuwa malengo ya Serikali kwa reli hiyo yalikuwa kurahisisha na kupunguza gharama za usafirishaji wa karatasi kutoka kiwandani hapo kuelekea maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Kiwanda cha karatasi Mufindi kilibinafsishwa mwaka 2004 kikiwa na uzalishaji wa karatasi nyeupe na karatasi ngumu kikiwa na uwekezaji uliofanywa na Baba wa Taifa wa dola za kimerekani milioni 360.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.