Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mhe. Dkt. Festo Dugange, ametoa maagizo kwa Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri kuhakikisha wanasimamia kwa ukamilifu maendeleo ya michezo na sanaa mashuleni, kama sehemu ya mkakati wa Serikali wa kukuza vipaji vya wanafunzi kupitia mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA.
Akizungumza wakati wa kufunga mashindano ya kitaifa ya UMITASHUMTA na UMISSETA yaliyofanyika mkoani Iringa, tarehe 29 Juni 2025, Dkt. Dugange aliwataka maafisa hao kutekeleza maagizo ya Serikali kwa vitendo ili kuimarisha michezo kuanzia ngazi ya shule za msingi hadi Sekondari.
"Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri, simamieni kwa nguvu shule za michezo na shule za amali katika maeneo yenu. Hakikisheni mnaweka walimu wenye taaluma ya michezo na sanaa katika shule hizo na kuwawezesha kwa kuwapatia vifaa muhimu vya kufundishia," alisisitiza Dkt. Dugange.
Aidha, alieleza kuwa Mikoa iliyowekeza katika shule maalum za michezo (vitalu) imeonesha mafanikio makubwa kwenye mashindano ya mwaka huu, jambo linalothibitisha kuwa uwekezaji sahihi katika michezo huzaa matokeo chanya.
Kuhusu miundombinu, Dkt. Dugange amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeshaanza kutekeleza mpango wa kuboresha miundombinu ya michezo katika shule teule 56 za Sekondari kwa kujenga na kukarabati viwanja pamoja na ununuzi wa vifaa vya michezo.
"Tathmini tayari imekamilika katika shule saba kutoka mikoa saba, na sasa hatua ya kutangaza zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi inaendelea," alisema Dkt. Dugange.
Vilevile, alisisitiza umuhimu wa michezo katika maendeleo ya kitaaluma na kijamii kwa wanafunzi, akieleza kuwa michezo hujenga nidhamu, huongeza ujasiri, kuboresha afya na kuchangia ongezeko la mahudhurio shuleni.
Katika hatua nyingine, aliagiza Maafisa Elimu kuhakikisha maeneo ya shule yaliyotengwa kwa ajili ya michezo hayaingiliwi na matumizi mengine, huku akihimiza ushirikiano na wadau wa sekta binafsi katika kuanzisha vituo vya michezo na akademia mashuleni.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.