Mikoa ya nyanda za juu kusini imetakiwa kudumisha umoja katika kufanikisha maonesho ya Utalii Karibu Kusini na shughuli za viwanda vidogo mwaka 2017.
Wito huo umetolewa na mwenyekiti wa kikao cha viongozi wakuu wa mikoa ya nyanda za juu kusini, Amina Masenza alipokuwa akifungua kikao cha pamoja cha maandalizi ya maadhimisho ya maonesho ya Utalii Karibu kusini na maonesho ya shughuli za viwanda vidogo (SIDO) kilichofanyika katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha jana.
Masenza alisema kuwa kanda ya nyanda za juu kusini inatakiwa kujipambanua kupitia utofauti wa kiutalii uliopo. “Tunayo maonesho ya Utalii Karibu Kusini kwa mikoa ya nyanda za juu kusini yatakayofanyika mkoani Iringa. Naomba waheshimiwa wakuu wa mikoa tushikaname kwa dhati ili jambo hili lifanikiwe” alisema Masenza. Aliongeza kuwa ikitokea kiongozi mmoja miongoni mwao akajiondoa atakuwa anaichelewesha kanda ya nyanda za juu kusini kufunguka kimaendeleo kupitia utalii. Alisisitiza kuwa ushirikiano wa pamoja ni msingi imara wa kufanikisha maonesho ya utalii na shughuli za viwanda kwa ukanda huo.
Katika salamu za mkuu wa mkoa wa Songwe, Luteni (Mst) Chiku Galawa alisema kuwa nyanda za juu kusini kuna fursa nyingi na kubwa za kiutalii. “Mwanzo ni mgumu siku zote. Fursa zilizopo ni nyingi na kubwa, kuanzia ziwa Tanganyika, ziwa Rukwa, Hifadhi za Mahale, Katavi, Ruaha, Kitulo, Selous kuna fursa nyingi na tofauti za kitalii” alisema Luteni Galawa. Aliongeza kuwa katika kufikia mafanikio, kazi ya ziada lazima ifanyike. “Ndugu zangu, tunahitaji kujitoa na kuonesha dhamira ya kweli. Lazima fursa tuzitengeneze sisi wenyewe, tusisubiri watu wa nje” alisema Luteni Galawa.
Maadhimisho ya Utalii Karibu Kusini na maonesho ya shughuli za viwanda vigodo (SIDO) yataanza tarehe 29/9/2017-2/10/2017 katika uwanja wa Kichangani- Kihesa Manispaa ya Iringa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.