Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Jumla ya mikataba 18 imesainiwa na wazabuni walioshinda zabuni yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 3 mkoani Iringa.
Kauli hiyo ilitolewa na Mratibu wa Wakala wa Barabara za vijijini na mijini (TARURA) Mkoa wa Iringa, Mhandisi Juma Wambura katika taarifa fupi ya TARURA iliyowasilikswa kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hafla fupi ya utiaji saini mikataba ya ujenzi wa barabara na vivuko baina ya TARURA na wakandarasi katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Iringa jana.
Mhandisi Wambura alisema TARURA mkoa wa Iringa ilitangaza miradi ya barabara ya halmashauri zote za mkoa. “Mhe. mkuu wa mkoa, TARURA Mkoa wa Iringa ilitangaza miradi ya barabara ya halmashauri zote za mkoa jumla ya zabuni 26 zenye thamani ya shilingi bilioni 6.5 ambayo leo utaishuhudia mikataba 18 ikisainiwa na wazabuni walioshinda baada ya mchakato mzima wa manunuzi kukamilika yenye thamani ya shilingi bilioni 3.56” alisema mhandisi Wambura. Alisema kuwa mikataba minane itasainiwa baada ya taratibu za manunuzi kukamilika.
Mratibu wa TARURA mkoa aliwaasa wazabuni hao kutekeleza miradi hiyo kwa weledi na ufanisi mkubwa pasipo kuchelewesha kama utaratibu wa miaka ya nyuma ulivyokuwa. “Aidha, ninawakumbusha wazabuni kuacha mazoea ya kutekeleza kazi chini ya kiwango kwa visingizio mbalimbali. TARURA haitamvumilia mkandarasi yeyote atakayezembea katika utekelezaji wa miradi hii” alisema mratibu wa TARURA. Aliwahakikishia wakandarasi kupata ushirikiano unaostahili katika kutekeleza majukumu yao.
Wakala wa barabara za vijijini na mijini (TARURA) ulianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya wakala za serikali sura 245 na kutangazwa katika Gazeti la serikali Na. 211 la tarehe 12/05/2017.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.