Mkuu wa Mkoa Iringa atoa maagizo mazito kwa Jamii Kupambana na Ukatili kwa Wanawake na Watoto, Atoa Maelekezo kwa Wakuu wa Wilaya na Wadau Mbalimbali
Akitoa maelekezo hayo katika kikao kilichoandaliwa na Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Jinsia na Wanawake na Watoto, Mheshimiwa Ally Hapi amesema, kuna umuhimu wa kupitia upya waganga wote wa jadi waliopo Mkoani humo, kuacha mila na desturi zilizopitwa na wakati, kuacha mambo ya kishirikina na ulevi wa kupindukia.
Mheshimiwa Hapi amesema mambo haya huchangia sana kufanya ukatili kwa wanawake na watoto. Akitoa mfano akasema mwanaume akishalewa anaweza kumpiga mke wake bila sababu. Utamaduni wa kupiga mwanamke umepitwa na wakati, mwanamke anatakiwa kupewa mapenzi, kubembelezwa na kupewa mahaba. Pia mtu akishaenda kwa mganga wa jadi kutafuta utajiri, ataambiwa akabake mtoto.
Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Watoto wameandaa mpango unaoitwa MTAKUWWA, ambao unafadhiliwa na UNICEF, mpango huu wa mawasiliano utasaidia kupunguza ukatili kwa wanawake na watoto. Pamoja na jitihada za UNICEF lazima jamii ipewe elimu juu ya mambo haya ya ukatili wa wanawake na watoto.
Ameongeza kuwa, hata wanaume huwa wanafanyiwa ukatili japo huwa hawasemi. Pia wazazi hatuna desturi za kuangalia watoto wetu pindi wanapotoka shule au kucheza sehemu mbalimbali. Kwani imebainika kuwa asilimia kubwa watoto hubakwa, kulawitiwa wakiwa wanatoka kwenye masomo ya ziada (Tuition), vibanda wanavyoonesha sinema na hata kumtuma mtoto nyakati za usiku kwenda dukani au sehemu mbalimbali.
Amesisitza tena, kila shule kuwe na mwalimu wa malezi ambaye atakuwa akiwaangalia na kuwasikiliza watoto pindi wanapokuwa wamepatwa na jambo kama hili. Hii itasaidia watoto kueleza matatizo yao bila uoga.
Ameongeza kwa kusema kuwa, nilipoenda kutembelea gerezani, wafungwa 30 waliofungwa maisha kwa kesi za kufanya ukatili. Pia takwimu za ubakaji, ulawiti na ukatilili wa kingono kuanzia Januari hadi Novemba, 2019 kesi zilizojulikana ni watoto 404 na wanawake 37 ambao wamefanyiwa ukatili. Jambo hii la ukatili linasababisha ongezeko la maambukizi ya UKIMWI, kwani Mkoa upo katika nafasi ya 11.3% na 43% ya udumavu hivyo bado tuna kazi kubwa ya kupambana vita hivi. Tatizo hili linachangiwa na mambo ya mila na desturi, Ushirikina, ulevi wa kupindukia.
Mwisho Mheshimiwa Hapi amesisitiza kuwa, jamii na wadau itoe macho katika maeneo ya kuonesha sinema, kwenye masomo ya ziada (tuition), waganga wa jadi ili ijulikane nini kinaendelea katika maeneo hayo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.