Mkuu wa Mkoa wa Iring Mhe. Queen Cuthbert Sendiga amezindua kampeni ndogo ya chanjo ya UVIKO-19 Mkoani Iringa ambayo ina lengo la kuongeza kasi ya uchanjaji.
Mhe.Sendiga amesema kuwa Mkoa wa Iringa ni moja kati ya mikoa inayotekeleza zoezi la uchanjaji chanjo ya UVIKO-19 ili kuwakinga wananchi dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19. Chanjo za UVIKO-19 zimeidhinishwa na shirika la Afya Duniani (WHO) kwa ajili ya Mapambano ya Ugonjwa wa UVIKO-19. Chanjo hizi zinapunguza uwezekano wa mtu kuambukizwa ugonjwa UVIKO-19 na hata mtu akiambukizwa hupunguza uwezekano wa kulazwa na kufa.
Aidha Mkuu wa mkoa wa Iringa amesema Mpaka sasa mkoa wa Iringa Umepokea chanjo za aina tano ambazo ni Janssen, Pfizer, Moderna, Sinovac na Sinopharm. Chanjo hizi zimeidhinishwa na serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kutumika nchini.
Aidha ameendelea kwa kusema kuwa, Baada ya Mafanikio makubwa kupatikana katika awamu ya kwanza ya mpango jumuishi harakishi wa uchanjaji chanjo ya UVIKO-19 Serikali kupitia Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI ilizindua Awamu ya pili ya mpango shirikishi na harakishi wa uchanjaji chanjo ya UVIKO-19 mnamo tarehe 22 Desemba 2021 Mkoani Arusha. Lengo la mpango huu ni kuongeza kasi ya uchanjaji kuelekea kufikia asilimia 70 ya watanzania ifikapo Desemba 2022.
“Kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari 2022 hadi tarehe 18 Julai 2022 mkoa umepokea chanjo za UVIKO-19 495,307 (Janssen 238035, Pfizer 161650, Sinopharm 51832, Sinovac 31500 na Moderna 12290). Uchanjaji chanjo ya UVIKO-19, umendelea kufanyika na kwa sasa mkoa unatekeleza kampeni ya uchanjaji chanjo ya UVIKO-19 iliyoanza tarehe 1 Juni 2022 hadi 30 Septemba 2022. Hadi kufikia tarehe 18 Julai 2022 mkoa umechanja jumla ya watu 133,497 sawa na asilimia 19.8 ya walengwa 671,974.” Mhe. Queen Sendiga.
Na hivyo Kuanzia tarehe 20 Julai 2022 hadi kufikia 24 Julai 2022 tutakuwa na kampeni ndogo ya uchanjaji chanjo ya UVIKO-19 inayolenga kuchanja wateja 100,000. Kufikia malengo haya kila halmashauri inatakiwa kuchanja wateja zaidi ya 2500 kwa siku.
Mhe. Queen Sendiga amemaliza kwa kuwahamasisha wananchi wote walio na umri wa miaka 18 na kuendelea ambao bado hawajapata chanjo ya UVIKO-19 wapate chanjo hii katika kipindi hiki cha kampeni. Pia wananchi waliopata dozi ya kwanza wafike katika vituo vya kutolea huduma za chanjo kupata dozi ya pili ili miili yao iweze kuwa na kinga kamili.
Kwa chanjo ya Sinopharm dozi ya pili inatolewa siku 28 baada ya kupata dozi ya kwanza na kwa chanjo ya Pfizer au Moderna dozi ya pili inatolewa kuanzia siku ya 21 hadi 28 baada ya kupata dozi ya kwanza. Kwa sasa mkoa una jumla ya vituo 259 vinavyotoa huduma za chanjo. Pamoja na uchanjaji katika vituo watoa huduma wanatumia huduma za mkoba ili kuwafikia wananchi popote walipo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.