Mheshimiwa Hapi ameyasema hayo katika kikao cha Wafanyabiasha/Wawekezaji Wilayani Mufindi tarehe 19/1282019 ikiwa ni moja ya majukumu yake katika kuhakikisha Mkoa wa Iringa unakuwa kiuchumi.
Akifungua kikao hicho Mheshimiwa Hapi amesema, kupitia uwekezaji nchi yetu inaweza kuongeza uchumi katika pato la Taifa, hivyo ni muhimu ikafahamika changamoto za wawekezaji, japo zingine zinafahamika. Dhamira ya Mkoa wa Iringa ni kutatua matatizo na vikwazo mbalimbali vinavyowakabili wawekezaji ili kumsaidia Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli katika kufanikisha kuleta wawekezaji nchini.
Mheshimiwa Hapi katika kukemea amesema, kuna baadhi ya Taasisi za Serikali zimekuwa mwiba kwa wawekezaji kwa kufanya kazi bila kufuata taratibu na kanuni za nchi. Baadhi ya Taasisi hizo huenda kwenye viwanda na kukusanya kodi wakiwa wameshika bunduki, Mheshimiwa Rais amepiga marufuku nchi nzima, kwani wafanyabiashara wamekuwa wakitishika sana, wanapoona bunduki hupoteza ufanisi wa kazi.
Wawekezaji hawa wakiwa wanahudumiwa vizuri hasa raia wa kigeni, wanaweza kutuma ujumbe kwenye nchi zao kuwa Tanzania ni mahali salama kwa uwekezaji. Ni majukumu ya Mkuu wa Mkoa kusimamia wajibu na sheria za nchi.
Mheshimiwa Hapi ameelekeza kuwa, kama Taasisi inakwenda kukagua viwanda, ni lazima Mkuu wa Wilaya husika apate taarifa, na watoe sababu wanakwenda kufanya nini, pia mwenye kiwanda lazima ajulishwe. Ikigundulika kuna makosa madogo huwa wanasema ‘funga kiwanda baada ya masaa 24’, sasa ni marufuku kiwanda kufungwa hadi Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa atakapojiridhisha kufunga kiwanda hicho kwa sababu husika.
Pia Mheshimiwa Hapi ameutaka uongozi wa TFS kutoa vibali vya kudumu kwa wawekezaji wenye sifa na vigezo na siyo kwa watu wachache tu kama ilivyo sasa hivi.
Amesisitiza kuwa, Halmashauri zote zitenge maeneo kwa ajili ya viwanda kwa wawekezaji, kuanzia sasa kila Mkurugenzi wa Halmashauri katika vikao vyetu ataeleza ametenga vipi maeneo hayo.
Akihitimsha kikao hicho Mheshimiwa Hapi amesema, Wilaya ya Mufindi ina neema kubwa ya uwekezaji viwanda, wasaidie wageni ili wawekeze kwa wingi bila bughudha. Pia amewaonya watu wa mazingira kufanya opereshini ya kukagua mifuko ya plastiki ambayo kwa sasa inatumika kwa kasi sana kama vifungashio.
Imetolewa na Ofisi ya Habari Mkoa,
Humphrey Kisika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.