Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-Iringa
Moto wa Iringa mpya kuunguza watumishi wa Serikali wazembe na wanaoingia ofisini muda wanaotaka mkoani Iringa.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe Ally Hapi alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi wa Tarafa ya Kibengu katika siku ya tatu ya ziara yake ya Tarafa kwa Tarafa mkoani Iringa leo.
Mhe Hapi alisema kuwa kutokana na utendaji kazi wa mazoea, wapo baadhi ya watumishi wanaoingia ofisini muda wanaotaka wao. “Moto wa Iringa mpya utakwenda kuwaunguza watendaji hao wote. Bahati nzuri mimi siyo mtu wa kukaa ofisini, nimeamua kuzunguka Tarafa zote 15 za Mkoa wa Iringa ili kuwasha moto huu. Hakika hautamuacha mtumishi wa aina hiyo salama”. Serikali ya Mhe Dkt John Pombe Magufuli imetoa fedha nyingi kuwaletea maendeleo wananchi, wapo watumishi wamegeuka mchwa, wanaotafuna fedha za miradi ya maendeleo ya wananchi. “Nimekuja mwenyewe kukagua miradi hiyo. Nataka niwahakikishie ndugu zangu wananchi kuwa watumishi wa aina hiyo hawatabaki salama” alisisitiza Mhe Hapi.
Katika kuhakikisha watumishi wa Serikali wanafanya kazi, aliagiza kuwa kila mtumishi wa Serikali kutoa taarifa ya kila wiki ya utekelezaji wa majukumu yake ya kazi. “Taarifa hizo zitakuwa za aina mbili. Aina ya kwanza ni kazi alizofanya wiki iliyopita na aina ya pili ni kazi atakazotekeleza wiki ijayo” alisema Mhe Hapi.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa yupo katika siku yake ya tatu ya ziara ya Tarafa kwa Tarafa akiwa katika Tarafa ya Kibengu amezindua nyumba moja ya walimu ya familia sita katika shule ya sekondari Ilogombe, kukagua ujenzi wa bweni la wanafunzi na miundombinu ya shule ya sekondari Kihansi na kufanya mkutano na wananchi wa Tarafa ya Kibengu.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.