Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi inatekeleza agizo la serikali ya kuanzisha viwanda nchini ili kujenga Tanzania ya viwanda ifikapo mwaka 2025.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Wilaya ya Mufinsi, Allan Benard alipokuwa akisoma risala ya utii ya wananchi wa halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kwa Rais Dkt John Magufuli katika uwanja wa mkesha wa Mwenge wa uhuru katika Kata ya Igowole wilayani Mufindi.
Benard alisema kuwa halmashauri ya Wilaya ya Mufindi inatekeleza maagizo ya serikali katika sekta mbalimbali. “Kabla ya kampeni ya Kiwanda changu Wilaya yangu, halmashauri ilikuwa na jumla ya viwanda 29, vikubwa saba, vya kati vitatu na vidogo 19. Baada ya kampeni hii, viwanda vidogo 11 vimeongezeka na kufanya jumla ya viwanda kuwa 40, ambavyo vinatoa ajira kwa watu 3,788.
Akiongelea utoaji wa chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wasichana, alisema kuwa halmashauri inaendelea na utekelezaji wa chanjo hiyo. Alisema kuwa kamati ya afya ya wilaya na watoa huduma za afya 63 na walimu 192 walipatiwa mafunzo. “Zoezi la utoaji chanjo linaendelea ambapo mpaka sasa jumla ya wasichana 402 (98) kati ya walengwa 442 kwa mwezi wamechanjwa ambapo walengwa 5,308 wanatarajiwa kufikiwa kwa mwaka” alisema Benard.
Mwenge wa uhuru katika halmashauri ya Wilaya ya Mufindi umepitia miradi sita yenye thamani ya shilingi 9,199,229,136. Miradi hiyo ni kuweka jiwe la msingi ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa sekondari ya Igombavanu, kukagua msitu wa kupandwa wa halmashauri na kuzindua ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha mtili. Miradi mingine ni kuzindua ujenzi wa barabara ya lami Kitiru-Itulituli Km 14.977, mradi wa kilimo na mifugo wa wananchi na klabu ya wapinga rushwa sekondari ya Igombavanu.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.