Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe Ally Hapi ameanza ziara ya kutembelea Wilaya za Mkoa wa Iringa, akianza na Wilaya ya Kilolo.
Akiwa Wilayani Kilolo, alifanya kikao na Kamati ya Ulinzi na Usalama na kusisitiza umoja na mshikamano. Vilevile, aliitaka Kamati hiyo kuweka utaratibu wa kubadilishana taarifa kwa wakati ili ziwawezeshe kufanya maamuzi sahihi katika kazi zao.
Mkuu wa Mkoa alitembelea ofisi ya CCM Wilaya ya Kilolo na kufanya kikao na kamati ya siasa ya Wilaya hiyo. Aliomba ushirikiano katika kuijenga Iringa mpya. Aidha, aliomba umoja na ushirikiano kuendelea kudumishwa kwa mkuu we Wilaya, Mkurugenzi na wakuu wa idara katika kutekeleza Ilani ya CCM.
Mkuu wa Mkoa alifanya kikao na watumishi wa Wilaya ya Kilolo na kuwataka kuwa wamoja. "Natamani kujenga Iringa mpya yenye umoja, umoja baina ya viongozi na watumishi. Tunapanga pamoja na tunatekeleza pamoja. Msitangulize ubinafsi wenu bali tangulizeni umoja wenu" alisisitiza mhe Hapi.
Aidha, aliwataka watumishi kutambua kuwa vyeo vyao ni dhamana ambazo wamepewa kwa ajili ya kuwatumikia wananchi. "Kila mmoja lazima awaheshimu wananchi wa Kilolo. Tusiwajibu ovyo, wala kuwa na kiburi. Tuwasikilize na kuwahudumia. Wananchi hawa ndiyo walipa kodi na wanaotulipa mishahara" alisisitiza mhe Hapi.
Mkuu wa Mkoa alisisitiza uadilifu na kufanya kazi kwa haki na kuzingatia sheria. Alikemea vitendo vya rushwa na kusisitiza utunzaji wa siri za ofisi.
Mhe Hapi aliitaka halmashauri ya Wilaya ya Kilolo kujikita katika ukusanyaji mapato na kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima ya fedha za serikali.
Katika kikao na wazee wa Wilaya ya Kilolo, Mkuu wa Mkoa aliwataarifu wazee hao kuwa alienda kujitambulisha kwao na kuomba ushirikiano wao katika kufikia malengo ya serikali. Aliwahakikishia wazee hao kuwa watendaji wa serikali wataendelea kutoa huduma nzuri kwa wananchi ili waendelee kuiunga mkono nakuiamini serikali yao. "Nimewaagiza watendaji kuwafuata wananchi huko mlipo na siyo nyie kuja kuwafuata watendaji walipo" alisisitiza mhe Hapi.
Katika mkutano wa hadhara, aliwahakikishia wananchi kuwa watendaji watawahudumia na kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi kwa wakati. Aliwataarifu wananchi kuwa amewaagiza watendaji wa serikali kutoka ofisini na kuwafuata Wananchi katika maeneo yao na kutatua kero zao.
Mkuu wa mkoa yupo katika ziara yake ya wilaya kwa wilaya kwa lengo la kujitambulisha na kuelezea mwelekeo wa ujenzi wa Iringa mpya anayokusudia katika uongozi wake.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.