Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-Iringa
Serikali inajukumu la kutatua kero za wananchi wake ili wajikite katika shughuli za kujiletea maendeleo.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe Ally Hapi alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi wa Tarafa ya Sadan wilayani Mufindi leo katika siku yake ya nne ya ziara ya Tarafa kwa Tarafa kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi.
Mhe Hapi alisema “tumejipanga kusimamia na kutatua changamoto zinazowahusu wananchi wa Tarafa ya Sadan na Mkoa wa Iringa kwa ujumla. Kazi kubwa ya Serikali ni kuleta maendeleo kwa wananchi wake, kazi kubwa ya Serikali ni kutatua kero za wananchi wake, kazi kubwa ya Serikali ni kuwahudumia wananchi wake vizuri na kuhakikisha wanaridhika na huduma zinazotolewa na Serikali yao”. Mhe Rais amenituma kuja kuhakikisha wananchi wanafurahia huduma wanazopata kutoka kwa watendaji wa Serikali, aliongeza.
Mhe Rais, Dkt John Magufuli amedhamiria kuwaletea wananchi maendeleo. Amejipambanua kuwa ni Rais wa wanyonge. “Kazi kubwa aliyonituma ni kuhakikisha wananchi waliomchagua mwezi Oktoba, 2015 wanafurahia huduma zinazotolewa na Serikali yao. Mhe Rais amenituma nije kumsaidia kazi ya kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua katika Mkoa wa Iringa, amenituma nihakikishe wananchi wanapata huduma nzuri za afya, maji, elimu na miundombinu. Mhe Rais ameongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 30 hadi kufikia bilioni 250 kwa mwaka huu kwa lengo la kuhakikisha wananchim wanapata huduma bora za afya” alisema Mhe Hapi.
Akiongelea dhana ya Iringa mpya aliyoianzisha, Mkuu wa Mkoa alisema kuwa Iringa mpya inalenga kuhakikisha watumishi wote wa Mkoa wa Iringa wanachapa kazi na kutoka ofisini kwenda kuwahudumia wananchi katika maeneo yao. “Mhe Rais ndiye ndiye mkuu wa watumishi wote wa umma nchini. Wananchi ndiyo mabosi wetu. Yeye anakwenda kusikiliza kero za wananchi iweje kwa sisi tunaomsaidia? Sitarajii kuona ndani ya Iringa mpya kuna watendaji wa vijiji, wasiosoma mapato na matumizi kwa wananchi. Sitarajii kuona watendaji kata wenye majibu ya kifedhuli kwa wananchi. Hii tunayotaka kuijenga inaitwa Iringa mpya” alisisitiza Mhe Hapi.
Aidha, aliongeza kuwa anataka kuona Iringa mpya ambayo wakulima wanamatumaini kwa sababu wanatembelewa na mabwana shamba. “Tunataka Iringa mpya mbayo vijana wanawezeshwa kiuchumi kwa kupewa mikopo midogo na Halmashauri ili wanunue mashine za kumwagilia na kuchana mbao ili waanzishe viwanda vidogo. Vijana lazima wajisikie fahari kwamba Serikali yao inawajali na kuwatumikia” alisisitiza Mhe Hapi.
Iringa mpya ni watumishi wa Serikali kazi yao kubwa ni kuwahudumia vizuri wananchi. Chini ya Iringa mpya watendaji wanaitendea haki mishahara wanayolipwa na Serikali, aliongeza Mkuu wa Mkoa.
Akiwa katika Tarafa ya Sadani Mkuu wa Mkoa alikagua ujenzi wa tanki la maji kijiji cha Maduma, kukagua ufugaji wa nyuki, alikagua lambo la mifugo na shamba la matikiti maji la mwananchi. Shughuli nyingi alizofanya ni kukagua ujenzi wa hosteli ya sekondari Mgalo na kufanya mkutano na wananchi wa Tarafa ya Sadani na kusikiliza kero za wananchi.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.