Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Serikali ya awamu ya tano itaendelea kushughulikia kero za wafanyakazi na kuboresha maslahi ili wafanye kazi kwa kujituma na tija zaidi.
Kauli hiyo ilitolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Magufuli alipokuwa akihutubia mamia ya wafanyakazi waliofurika katika uwanja wa michezo wa Samora mjini Iringa katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani.
Dkt Magufuli alisema kuwa serikali yake itaendelea kushughulikia kero na kuboresha maslahi ya wafanyakazi nchini. “Leo ni siku ya wafanyakazi, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza wafanyakazi kwa mchango wenu mkubwa wa kuiletea nchi maendeleo. Hongereni sana”. Aidha, aliwataka watumishi hao kutanguliza nidhamu na uwajibikaji katika utendaji wao wa kazi. “Mtumishi akiwa mvivu na mzembe anakuwa ni mnyonyaji” alisema Dkt. Magufuli.
Kuhusu wafanyakazi kuhamishwa bila kulipwa stahili zao, Rais Dkt Magufuli alimuagiza waziri mkuu kuwasimamia wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa ambao bado wanahamisha wafanyakazi bila kuwalipa stahili zao. “Waziri mkuu nakuomba ulisimamie hilo. Hatuwezi kuwa tunatoa maagizo halafu mtu mwingine aendelee kufanya hivyo. Tulishatoa maagizo mtu asihamishwe bila kulipwa. Naagiza tena viongozi ndani ya serikali wasihamishe bila kulipa fedha za uhamisho. Ni matumaini yangu sitarudia tena kuzungumzia hili katika maisha yangu”.
Akiongelea malimbikizo ya watumishi, alisema kuwa serikali yake imelipa malimbikizo kwa watu 52,852 yenye thamani ya shilingi bilioni 86,323. Vilevile, aliwahakikishia watumishi kuwa wale wote wenye madai halali watalipwa haki zao. “Kwa hizi nyuso za furaha mnazonionesha leo, ningekuwa na hela kwenye chungu zimebaki pale, leo ningetamka tu. Lakini nikitamka ntazitoa wapi? Nina mpango wa kuajiri wafanyakazi 52,000 ntawalipa nini? Dhamira yangu inanituma kwamba kusubiri ni kitu kizuri. Hebu tujenge miundombinu na kuajiri hawa 52,000. Tutaendelea kulipa viporo vya madeni hadi viishe” alisema Dkt Magufuli.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.