Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Serikali imeamua kudhibiti mfumuko wa bei za bidhaa ili kuwapunguzia ugumu wa maisha wafanyakazi nchini.
Kauli hiyo ilitolewa na Rais Dkt John Magufuli alipokuwa akiongea na wafanyakazi katika sherehe za Mei Mosi kitaifa zilizofanyika katika uwanja wa Samora mjini Iringa.
Dkt Magufuli alisema “nachotaka kuwaambia ndugu zangu, nawapenda wafanyakazi. Nilitamani mwaka huu kupandisha mishahara, lakini baada ya kuona hizi changamoto tulizonazo nikaona tuzimalize kwanza na kuthibiti mfumuko wa bei ya bidhaa. Naomba mnielewe ndugu zangu wafanyakazi”. Aliongeza kuwa serikali yake imefanikiwa kudhibiti mfumko wa bei hadi kufikia asilimia 3.9.
Rais Dkt Magufuli alisema kuwa serikali yake imejikita katika kutekeleza miradi ya maendeleo yenye matokeo makubwa kwa taifa. Alisema kuwa miradi hiyo itasaidia kuongeza fedha kwa serikali na kwa wananchi.
Dkt Magufuli ilizitaja shughuli zinazotekelezwa na serikali yake kuwa ni kutoa elimu bila malipo kwa wanafunzi wa elimu msingi. Alisema utekelezaji huo unaigharimu serikali shilingi bilioni 23.8 kila mwezi, ikiwa imetoa shilingi bilioni 714 tangu aingie madarakani. Shughuli nyingine aliitaja kuwa ni ulipaji wa madeni ya mifuko ya hifadhi ya jamii yaliyofikia shilingi trilioni 1.6 ambapo jumla ya shilingi trilioni 1.4 zimelipwa na serikali yake mpaka sasa.
Serikali yake imelipa zaidi ya shilingi trilioni mbili kwa kipindi cha miaka miwili, zikiwa ni madeni ya nje.
Kwa upande wa mishahara, alisema “mishahara tunalipa shilingi bilioni 564.501 baada ya kutoa wafanyakazi hewa, zamani tulikuwa tunalipa shilingi bilioni 777”.
Maeneo mengine aliyataja kuwa ni kuongeza mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, kujenga bandari ya Mtwara, miradi ya maji, ukarabati wa reli na ujenzi wa rada. Miradi mingine ni ujenzi wa meli, ununuzi wa ndege, ujenzi wa miundombinu ya umeme na ujenzi wa mradi wa Stigler's Gorge.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.