WAJASIRIAMALI WANAKABILIWA NA TATIZO LA KUJITANGAZA
Na Dennis Gondwe, IRINGA
Wajasiriamali wengi wanakabiliwa na tatizo la kujitangaza jambo linalosababisha washindwe kufikia masoko ya bidhaa kwa urahisi.
Kauli hiyo ilitolewa na meneja wa SIDO Mkoa wa Ruvuma, Martin Chang’a alipokuwa akiongea na waandishi wa habari waliotembelea banda la SIDO katika maadhimisho ya siku ya utalii duniani, maonesho ya utalii karibu kusini na maonesho ya shughuli za viwanda vidogo (SIDO) kwa mikoa ya nyanda za juu kusini yaliyofanyika mkoani Iringa hivi karibuni.
Chang’a alisema kuwa wajasiriamali wengi wanajuhudi ya kuzalisha bidhaa nzuri kutokana na mafunzo wanayoyapata kutoka SIDO, changamoto ni jinsi ya kufikia masoko. Alisema kuwa tatizo kubwa linalowakabili wajasiriamali ni mbinu za kujitangaza na kutangaza bidhaa zao. “Mbinu za kujitangaza ni muhimu sana kwa wajasiriamali kwa sababu zinawasaidia katika kufikia masoko kirahisi. Kwa kuona tatizo hilo, SIDO tumetoa mafunzo ya jinsi ya kuboresha mbinu za kujitangaza kwa wajasiriamali wanaoshiriki maonesho haya ili kuwasaidia kuwa na uwezo wa kujitangaza” alisema Chang’a.
Akiongelea lengo la maonesho hayo kwa upande wa SIDO, Meneja wa SIDO mkoa wa Ruvuma alisema kuwa maonesho hayo yanalenga kuwatangaza wajasiriamali na shughuli wanazofanya ili zijulikane kwa watu. Aliongeza kuwa, maonesho hayo yanawawezesha wajasiriamali kukutana na kubadilishana uzoefu katika shughuli zao.
Maadhimisho ya siku ya utalii duniani, maonesho ya utalii karibu kusini na maonesho ya shughuli za wajasiriamali wa SIDO yamehusisha mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma, Rukwa, Songwe, Mwanza, Pwani, Dar es Salaam, Geita, Lindi, Morogoro, Kilimanjaro, Tabora na nchi ya Kenya. Maonesho hayo yamehusisha mashine mbalimbali, bidhaa za usindikaji, bidhaa zilizosindikwa, bidhaa za ngozi, kazi za mikono na dawa.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.