Watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa wametakiwa kuacha ushabiki wa kisiasa katika kutekeleza majukumu yao ya kiserikali katika kuwahudumia wananchi.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipofanya ziara ya kuwatembelea wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini katika mtaa wa Ngelewala uliopo Kata ya Mwangata, Manispaa ya Iringa leo.
Masenza alisema kuwa ushabiki wa kisiasa unaofanywa na watendaji wa Halmashauri unarudisha nyuma maendeleo ya wananchi. “Watendaji acheni ushabiki wa kisiasa. Baadhi yenu mmejiingiza kushabikia vyama vya CCM na Chadema. Anayetaka kufanya ushabiki wa kisiasa aache kazi na kwenda kwenye majukwaa kufanya siasa” alisema Masenza. Alisema kuwa wananchi wanahitaji maendeleo na watendaji wameajiriwa ili kuwasaidia wananchi kufikia maendeleo yao.
Aidha, aliwataka watendaji wa mitaa kusimamia ujenzi wa vyoo bora katika mitaa ya Manispaa. “Watendaji wa mitaa simamieni ujenzi wa vyoo bora kwa kila kaya katika Manispaa. Wanufaika wa TASAF wasipokuwa na vyoo bora kipindupindu kikiingia watakufa” alisema Masenza.
Wakati huohuo, mkuu wa mkoa aliwataka maafisa maendeleo ya jamii na maafisa kilimo kusimamia maendeleo ya wanufaika wa mpango wa TASAF. “Maafisa kilimo, mifugo na maendeleo ya jamii kujitathmini wameshiriki kiasi gani katika kubadilisha hali za maendeleo ya wananchi hawa” alisema Masenza.
Mpango wa kunusuru kaya masikini katika Manispaa ya Iringa ulizinduliwa tarehe 6/1/2015.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.