Na ofisi ya mkuu wa mkoa, Iringa
Watendaji wa serikali mkoani Iringa wametakiwa kuwapa kipaombele viongozi wa dini wanapofika katika ofisi za umma kupata huduma mbalimbali.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Ally Hapi alipokuwa akiongea na viongozi wa dini wa mkoa wa Iringa katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa Mkoa.
Hapi alisema “mimi naheshimu sana viongozi wa dini katika kazi na utumishi wetu. Sitataka viongozi wa dini wapange foleni kwenye mabenchi ya ofisi za umma. Namuelekeza Katibu Tawala Mkoa na wakuu wa Wilaya lazima viongozi hawa wasikilizwe kwa haraka wanapofika katika ofisi za umma. Mambo ya viongozi wa dini yapewe kipaombele”. Viongozi wa dini wanajukumu kubwa la kuwahudumia wananchi na kuliombea taifa, wasikilizwe haraka hoja zao kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.
Hapi alisema kuwa uongozi wake una nia thabiti ya kuleta maendeleo kwa mkoa wa Iringa. “Tunatamani kufanya mambo makubwa katika mkoa wetu, tunatamani kukuza utalii katika mkoa wetu ukizingatia tuna hifadhi kubwa ya taifa ya Ruaha, tunatamani kuhamasisha ujenzi wa viwanda vingi mkoani Iringa, tunatamani kuuza unga nje ya nchi badala ya kuuza mahindi ili vijana wetu wapate ajira ndani ya mkoa” alisisitiza Hapi.
Wakati huohuo, Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Happines Senenda alisema kuwa alishangazwa na wingi wa muitikio wa viongozi hao wa dini katika kikao na mkuu wa Mkoa. “Hii imenidhihirishia kuwa wana Iringa ni wamoja” alisema Senenda. Hakika tunaanza na Mungu, aliongeza.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa alifanya kikao rasmi na viongozi wa dini ili kujitambulisha na kuomba ushirikiano wao katika kufanikisha malengo ya serikali katika mkoa wa Iringa
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.