Mamlaka za serikali za mitaa mikoa ya nyanda za juu kusini zimetakiwa kuweka utaratibu wa kupima afya katika Kata ili wananchi wengi wanufaike na huduma za afya na kukabiliana na magonjwa.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipotembelea banda la Halmashauri ya wilaya ya Kilolo katika maonesho ya Nanenane kwenye uwanja wa John Mwakangale mjini Mbeya jana.
Masenza alizitaka Halmashauri kuweke utaratibu wa kutembelea Kata na kutoa elimu ya afya na upimaji magonjwa mbalimbali badala ya kusubiri kupima katika maonesho ya Nanenane yanayofanyika mara moja kila mwaka. “Wekeni utaratibu wa kutembelea Kata na kupima afya wananchi hasa wakina mama wanapohudhuria kliniki na kuwapa elimu ya afya na lishe. Utaratibu huu utasaidia kuokoa maisha ya watu na kuimarisha hali zao za lishe kwa sababu wananchi wengi hawapati huduma hizo kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na umbali” alisema Masenza.
Masenza alisema kuwa mikoa ya nyanda za juu kusini inakabiliwa na tatizo la lishe pamoja na kuwa ni mikoa yenye kiwango kikubwa cha uzalishaji wa mazao ya chakula. Alizitaka mamlaka za serikali za mitaa na wadau wote kuweka mikakati ya kuhakikisha elimu inaendelea kutolewa kwa wananchi juu ya uchanganyaji wa chakula katika kutengeneza mlo kamili. “Juhudi za pamoja zitasaidia kukusanya rasilimali na kuzitawanya kwa mujibu wa maeneo ya kipaumbele na uhitaji kuliko kila mmoja kufanya peke yake. Ushirikiano huu utarahisisha kuzibaini changamoto zilizopo na kuzipatia ufumbuzi wa pamoja” alisema Masenza.
Maonesho ya shughuli za wakalima Nanenane mwaka 2017 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo, “zalisha kwa tija mazao na bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi kufikia uchumi wa kati”.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.