IRINGA WATAHADHARISHWA MAJI YA MTO RUAHA
Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-IRINGA
Wananchi wa mkoa wa Iringa wametahadharishwa kutumia maji ya mto Ruaha kutokana na vipimo kuonesha kuwa maji hayo yanavimelea vya ugonjwa wa Kipindupindu.
Tahadhari hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, mheshimiwa Amina Masenza alipokuwa akiongea mahojiano ya moja kwa moja kwenye kipindi cha nyota ya asubuhi kinachorushwa na kituo cha redio Furaha cha mjini Iringa leo.
Mheshimiwa Masenza alisema “maji ya mto Ruaha siyo safi na salama. Baada ya kuyapima imegundulika yana vimelea vya ugonjwa wa Kipindupindu”. Hivyo, amewataka wananchi kuchukua tahadhari katika matumizi ya maji hayo.
Wakati huohuo, aliwataka wananchi wa mkoa wa Iringa kuongeza kasi ya ujenzi wa vyoo bora. Alisema kuwa choo bora ni kile kisichomruhusu mtumiaji kukutna na kile anachokitoa ili kisimsababishie maradhi. Alisema kuwa choo ni sehemu ya kupumzika hivyo, kinatakiwa kutayarishwa vizuri ili kumstiri anayekitumia kwa kuwa na nafasi ya kutosha na kuruhusu hewa ya kutosha kupita. Aliwataka wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali zinazohamasisha kujenga jamii yenye afya njema.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.