Akifungua kikao hicho Mheshimiwa Hapi amesema, marufuku kunywa pombe na kulewa saa za kazi, vilabu vya pombe vinavyofunguliwa wakati wa saa kazi vinasababisha watu walewe na kuwa wabakaji, kulawati watoto na kufanya ukatili wa kingono. Amesema akikuta kijiji kuna kilabu cha pombe saa kazi, Mtendaji wa kijiji atachukuliwa hatua kali, hadi Mtendaji wa Kata na Afisa Tarafa wa eneo hilo. Kuna taarifa baadhi ya watendaji wa vijiji kuwa huwa wanachukua fedha kwa watu wanaouza pombe ili watu hao waendelee na biashara zao za pombe. Mheshimiwa Hapi amesema, nahitaji taarifa kila wiki nipate taarifa ya ulevi unaofanyika katika kila kijiji/mtaa ambao huwa wanalewa saa kazi. Kwani sehemu kubwa ya watu wanaofanya ulevi ni chanzo cha ubakaji, ukatili wa kingono na ulawiti kwa watu.
Amesema kuwa, wanawake walifanyiwa ukatili ni kama hivi: Iringa Manispaa ni watu 6, Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo ni watu 16, Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi ni watu 15,Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ni watu 16, ambapo takwimu hizi ni kutoka Januari hadi Novemba 31, 2019 jumla ni 37. Idadi hii ni kubwa sana kwa kesi ambazo zimefika katika vyombo vya usalama.
Ametoa maelekezo kwa Jeshi la Polisi, watendaji na viongozi wa vijiji, kuwakamata wazazi ambao wanafanya makubaliano ya kuficha ambao ya ukatili wa kingono kwa watoto. Pia wazazi ambao watoto wao wamebakwa, kulawitiwa na kufanyiwa ukatili wa kingono na hawajatoa taarifa katika vyombo vya usalama au sehemu yoyote lazima wakamatwe na watiwe hatiani.
Alipokutana na Wadau wa Elimu Mkoani humo Mheshimiwa Hapi alisema, kila shule ya msingi, sekondari au chuo cha ufundi kuwe na Walimu wa Malezi, ambao watapatiwa mafunzo/semina maalumu kwa kushirikiana na Ustawi wa Jamii na Dawati la Jinsia, ili iwe rahisi watoto wetu wapate nafasi ya kueleza matatizo wanayokumbana nayo. Kila shule itenge chumba kidogo ambacho atakaa mlezi huyu na kuweza kuwasikiliza watoto.
Ameongeza kusema kuwa, tatizo la watoto ambao wapo sekondari, Serikali inatoa elimu bure, lakini baadhi yao hawajulikani walipo. Yaani watoro sugu. Jumla ya watoto 777 ikiwa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ni watoto 481, Mafinga Mji watoto 27, Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi watoto 302, na Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo ni watoto 108 na Iringa Manispaa ni watoto 68. Nafikiri watoto hawa ndiyo wanaoingia katika kundi la kubakwa na kulawitiwa, kwa hata taarifa zao hazipo. Sasa fedha za elimu bure zinapotea bure, watoto wanaobakwa ni sehemu ya hawa chokoraa. Pia yawezekana watoto hawa wanachukuliwa na kwenda kufundishwa uhalifu huko msituni.
Amemaliza kwa kusema kuwa natoa maagizo kwa Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Maafisa Elimu na Jeshi la Polisi: watoto hawa wazazi wao wanajulikana, kuna uongozi kwa kila kijiji, watafutwe popote walipo. Kama kuna mzazi hatatoa ushirikiano lazima akamatwe na atiwe hatiani. Taarifa zao ni muhimu sana kuzipata, tujue kama mtoto ameozeshwa, amefariki au amehama lazima tujue. Ni muhimu kuchukua hatua madhubuti, vinginevyo janga la UKIMWI halitaisha katika Mkoa wa Iringa. Natoa muda wa mwezi mmoja nipate taarifa juu ya jambo hili, tarehe 17/12/2019 nipate ripoti ya jambo hili.
Amemaliza kwa kusema, nawapongeza Watendaji wote kwa kazi kubwa ambazo wanaendelea kuzifanya, jambo hili lazima lipewe kipaumbele ili kukuza Mkoa wa Iringa.
Imetolewa na Ofisi ya Habari Mkoa,
Humphrey Kisika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.