RC IRINGA APONGEZA JUHUDU ZA SAVE THE CHILDREN
Na.Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-IRINGA
Mkuu wa mkoa wa Iringa, mheshimiwa Amina Masenza amepongeza juhudi zinazofanywa na shirika lisilo la kiserikali la Save the Children kwa kuunga mkono juhudi za serikali za kuwahudumia wananchi wake.
Pongezi hizo alizitoa alipokuwa akiongea katika kipindi cha moja kwa moja cha nyota ya asubuhi kinachorushwa na kituo cha redio Furaha cha mjini Iringa leo.
Mheshimiwa Masenza alisema kuwa mkoa wa Iringa umeandaa kampeni ya kupima afya “afya check campaign” na kufadhiliwa na shirika la Save the Children. “Save the Children wamejipanga kutusaidia kwelikweli hivyo, tuwape ushirikiano mkubwa katika kutekeleza majukumu yao. Serikali inatambua na kuthamini mchango wa shirika hilo kwa ustawi wa afya za wananchi wetu. Kweli shirika hili linaunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais wetu Dr John Magufuli za kuhakikisha wananchi wake wanakuwa na afya njema ili washiriki katika ujenzi wa Taifa” alisema Mheshimiwa Masenza.
Akiongelea umuhimu wa kupima afya, mkuu wa mkoa alisema “mtu anayeogopa kujua afya yake ni mtu wa ovyo”. Alisema kuwa kupima afya ni ustaarabu na kuwataka wananchi kujitokeza kupima afya zao katika kampeni hiyo.
Aidha, aliwataka wakuu wa wilaya kuwasimamia madaktari katika wilaya zao ili wananchi waweze kupimwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Alisema kuwa upimaji huo katika wilaya utasaidia kuibua wagonjwa wa kifua kikuu na kuanzishiwa matibabu bure.
Mkoa wa Iringa katika kuadhimisha siku ya kisukari duniani inayoadhimishwa kila tarehe 14 Novemba uliamua kuadhimisha kwa kampeni ya kupima afya na uzinduzi wa ufunguzi wa kifua kikuu ngazi ya jamii. Uzinduzi tafanyika katika bustani ya Manispaa maarufu kama Garden kesho tarehe 18 Novemba, 2017.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.