Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Wakulima nchini wamekuwa wakipoteza zaidi ya asilimia 30 ya mavuno na kuwanyima wakulima kunufaika na jasho lao.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hotuba yake kwenye zoezi la uhamasishaji wa kupunguza upotevu na uharibifu wa zao la mpunga pamoja na kuhifadhi pamoja ili kuwa na soko la uhakika katika tarafa ya pawaga, wilayani Iringa.
Masenza alisema kuwa uhifadhi na utunzaji duni wa mazao umekuwa ukisababisha upotevu wa mavuno jambo linaloathiri kipato cha mkulima. “Takwimu zinaonesha kuwa upotevu ni takribani asilimia 30- 40 ya mavuno yote ya mkulima na hutokea baada ya mavuno. Hiki ni kiwango kikubwa sana ambacho kinawanyima wakulima uwezo wa kufaidika kutokana na jasho lao lakini pia kinaipa Wilaya, Mkoa na Nchi changamoto kubwa ya kuhakikisha uhakika endelevu wa chakula hapa nchini’ alisema masenza. Kwa kiasi kikubwa upotevu husababishwa na ukaushaji usioridhisha, mbinu duni za uvunaji, shambulio la wadudu na visumbufu” alisema Masenza.
Akiongelea uhifadhi wa mazao kwa pamoja ghalani, mkuu wa mkoa alisema kuwa serikali imekuwa ikichukua hatua kwa kushirikiana na wadau kukabiliana na tatizo la upotevu na uharibifu wa mazao. Hatua hizo alizitaja kuwa ni kuelimisha wakulima jinsi ya kudhibiti upotevu wa mazao baada ya kuvunwa, njia bora za uhifadhi pamoja na kujenga maghala bora. Kujenga maghala ya kuhifadhia mazao peke yake hakutoshi kudhibiti uharibifu huo. Uharibifu na upotevu wa mavuno hutokea tangu hatua ya kuvuna hadi kuandaliwa kuliwa, aliongeza.
“Serikali kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) wametenga fedha kwa ajili ya mradi wa kupunguza upotevu wa mpunga kabla na baada ya mavuno na kuongeza mnyororo wa thamani na soko la mchele kwa wakulima wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa” alisema Masenza.
Wakati huohuo, mkuu wa mkoa aliwaagiza viongozi wote wa vijiji, Kata na Tarafa wakiwepo Wenyeviti na Watendaji wa Vijiji, Watendaji wa Kata, Madiwani na Maafisa Tarafa wawe mfano wa kuanza kuhifadhi ghalani na kumpatia tarifa ya utekelezaji. Vilevile, Viongozi wafanye mikutano ya uhamasishaji kwa wakulima kila kijiji na sehemu ya kuuzia mpunga/mchele iwe ni katika maghala yaliyojengwa ili kuzuia wakulima wasindelee kupunjwa na wafanyabiashara kwa kuwapa bei ndogo.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.