Miradi ya Maendeleo ya Zaidi ya Bilioni 30 Kupitiwa na Mwenge wa Uhuru Iringa
Zaidi ya miradi ya maendeleo 46 yenye thamani ya shilingi bilioni 30.8 inatarajiwa kukaguliwa na Mwenge wa Uhuru mwaka huu katika Mkoa wa Iringa, ambao utakimbizwa umbali wa kilometa 625.1 kuanzia tarehe 28 Aprili hadi 3 Mei 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari leo April,24,2025 mjini Iringa, Mkuu wa Mkoa wa Iringa,Mhe. Peter Serukamba, amesema kuwa Mwenge wa Uhuru utaanza mbio zake mkoani humo ukitokea Mkoa wa Dodoma mnamo Aprili 28, 2025 kuanzia saa 12 asubuhi.
Kwa mujibu wa Mhe. Serukamba, amesema kuwa mwenge huo utakimbizwa katika halmashauri zote tano za Mkoa huo ambazo ni Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Kilolo, Mufindi, Halmashauri ya Mji Mafinga na Manispaa ya Iringa.
“Mwenge huu si tu unakuja kuhamasisha maendeleo bali pia kuhimiza mshikamano wa kitaifa, amani na uwajibikaji kwa viongozi na wananchi,” amesema Serukamba.
Ratiba ya mbio za Mwenge mkoani hapa itahitimishwa Mei 3, 2025 katika Uwanja wa Michezo wa Shule ya Msingi Idofi, ambapo sherehe ya makabidhiano ya mwenge kati ya mikoa ya Iringa na Njombe itafanyika.
Miradi itakayozinduliwa, kukaguliwa na kuwekewa mawe ya msingi inajumuisha ile inayotekelezwa katika sekta muhimu kama afya, elimu, maji, lishe, miundombinu pamoja na miradi ya uzalishaji mali inayolenga kuongeza kipato cha wananchi wa kawaida.
Aidha, Serukamba ametoa wito kwa wananchi wa Iringa kujitokeza kwa wingi kuupokea Mwenge wa Uhuru na kushiriki kikamilifu kwenye shughuli zitakazoambatana na Mwenge wa Uhuru, akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, utulivu na mshikamano wakati wote wa tukio hilo.
Kaulimbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni "Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu" ikilenga kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika mchakato wa kidemokrasia kwa njia ya amani,”
Mbio za Mwenge wa Uhuru hutoa fursa ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kutambua changamoto zilizopo, na kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.