Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Peter Serukamba amewasisitiza Watumishi wa mahakama nchini kuwa waadilifu na kuepuka rushwa kwani ni kikwazo katika kujenga Taifa bora.Ameyasema hayo Februari 03, 2025 wakati wa maadhimisho ya kilele cha siku ya sheria yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Mahakama Kuu ya Tanzania Mkoani Iringa.Mhe. Serukamba amesema kuwa wanasheria wanapaswa kupambana na Rushwa kwani ni Adui wa haki kwa kuwa watu wengi wanakosa haki zao kwa Sababu ya Rushwa.Aidha Mhe. Serukamba ameongeza kuwa wanapoongelea Dira ya 2050 wanapaswa kujenga jamii iliyo bora yenye haki,usawa na wasitoe wala kupokea rushwa ili pawepo na taifa lenye maendeleo.Pia Mhe. Serukamba ameeleza na kuomba kuwa kila mwananchi anapaswa kuwa na elimu ya sheria ili kuepuka migogoro na kufanya jamii kuwa na amani na utulivu ili kuwa na Taifa endelevu na lenye maendeleo katika nyanja tofauti tofauti.Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu Kanda ya Iringa, Dunstan Ndunguru wakati akisoma taarifa inayohusu maadhimisho hayo amefafanua kwamba mahakama katika kipindi cha wiki hiyo imefanikiwa kufanya maonyesho ya huduma zinazotolewa na mfumo wa haki za kisheria na namna wananchi wanavyoweza kutumia huduma hizo ili kulinda haki zao. Akiendelea kuzungumzia maadhimisho hayo Ndunguru amesema kuwa maonyesho hayo yalijumuisha utoaji wa elimu kuhusu sheria za familia, urithi, kazi, na haki za watoto, ikiwa ni njia mojawapo ya kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwaelimisha kuhusu masuala ya kisheria.Ikumbukwe kuwa maadhimisho hayo ya wiki ya sheria yalianza mkoani Iringa Januari 25 mpaka Februari mosi mwaka huu na kilele chake kikiwa ni leo Februari 03, 2025 huku Kauli mbiu ikiwa ni "Tanzania 2050 Nafasi ya Taasisi zinazosimamia Haki, Madai katika kufikia Malengo makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo".
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2025, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.