Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Serikali mkoani Iringa imewataka wakandarasi wa ujenzi wa miradi ya barabara kujipanga sawasawa katika kutekeleza miradi ya ujenzi ili idumu kwa muda mrefu.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hotuba yake ya halfa ya utiaji saini mikataba baina ya TARURA na wakandarasi katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa Mkoa jana.
Masenza aliwataka wakandarasi wote walioshinda zabuni za ujenzi wa barabara katika Mkoa wa Iringa kujipanga sawasawa. “Serikali imewekeza pesa nyingi katika ujenzi wa barabara kwa lengo la kujenga na kuimarisha barabara ili mwananchi aweze kunufaika na barabara hizo. Tumesikia katika taarifa ya mratibu wa TARURA Mkoa wa Iringa kuwa gharama za ujenzi wa barabara ni shilingi bilioni 3.56” alisema Masenza. Aidha, alitumia hafla hiyo kuwataka wakandarasi wote kufanya kazi kwa kuzingatia muda uliopangwa na viwango vya ubora wa kazi. Serikali haitamvumilia mkandarasi yeyote atakayefanya kazi chini ya muda uliopangwa kwenye mkataba wala kazi iliyofanywa chini ya kiwango, aliongeza Masenza.
Katika kuhakikisha ubora wa kazi za ujenzi, mkuu wa mkoa wa Iringa aliwataka mameneja wa TARURA wa halmashauri kuwasimamia wakandarasi ili watekeleze majukumu yao. “Serikali imeajiri mameneja wa TARURA katika halmashauri. Jukumu kubwa la mameneja hawa ni kuwasimamia wakandarasi ili watekeleze wajibu wao. Hivyo, mameneja wa halmashauri pia mjipange sawasawa kuhakikisha ubora na thamani ya fedha inapatikana” alisisitiza mkuu wa mkoa.
Mkuu wa mkoa alitoa wito wa kulipwa kwa wakati pindi wakandarasi watakapotimiza wajibu wao kwa kuzingatia vigezo vya ubora kwa mujibu wa mikataba iliyosainiwa. Alisema kuwa kuna wakati malipo ya wakandarasi yamekuwa yakicheleweshwa kutokana na uzembe na kutofuata taratibu. “Utekelezaji huo utawafanya kuongeza morari ya kazi na pia kuondoa malalamiko yasiyo ya lazima kwa Serikali” alisema mkuu wa mkoa.
Awali mratibu wa TARURA Mkoa wa Iringa, mhandisi Juma Wambura katika taarifa yake alisema kuwa TARURA Mkoa wa Iringa ilitangaza miradi ya barabara za halmashauri zote za Mkoa jumla ya zabuni 26 zenye thamani ya shilingi bilioni 6.5. “Leo utaishuhudia mikataba 18 ikisainiwa na wazabuni walioshinda baada ya mchakato mzima wa manunuzi kukamilika yenye thamani ya shilingi bilioni 3.56. Mhe. mkuu wa mkoa, mikataba takribani 8 itasainiwa baadae baada ya taratibu za manunuzi kukamilika” alisema mhandisi Wambura.
Mratibu huyo alisema kuwa lengo la TARURA ni kufanikisha dhima kuu ya Serikali kuwa miundombinu ya barabara inaboreshwa na kusonga mbele kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi ili iweze kuboresha uchumi wa wananchi.
TARURA mkoa wa Iringa inahudumia mtandao wa barabara wenye jumla ya Kilomita 4,601.25 inayojumuisha halmashuri tano za Manispaa, halmashauri za wilaya za Iringa, Kilolo, Mufindi na Mji wa Mafinga.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.