KIKAO CHA LISHE CHAONYESHA MAFANIKIO MKOANI IRINGA
Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Bi. Doris Kalasa, Leo Septemba 11, 2025 ameongoza kikao cha tathmini ya utekelezaji wa afua za lishe kwa kipindi cha Aprili hadi Juni 2025. Kikao hicho kimeudhuriwa na wadau mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu, afya, Maendeleo ya Jamii, na uchumi kwa lengo la kupitia hatua zilizochukuliwa katika kuimarisha hali ya lishe kwa watoto na wanafunzi mashuleni.
Katika kikao hicho, wadau wamejadili umuhimu wa kuendelea kuelimisha jamii umuhimu wa lishe bora mashuleni pamoja na kuwahimiza viongozi kuhakikisha vyakula vinavyouzwa mashuleni vinakuwa salama na vyenye ubora wa lishe. Hatua hii inalenga kuhakikisha wanafunzi wanapata mlo bora utakaosaidia kukuza afya na kuimarisha uwezo wao wa kujifunza.
Hata hivyo, Ripoti iliyowasilishwa imeonyesha kuwa hali ya lishe kwa watoto walio chini ya miaka mitano inaendelea kuimarika kutokana na mshikamano wa wadau katika kutekeleza afua mbalimbali. Aidha, imebainika kuwa mikakati inayotekelezwa imekuwa na mchango mkubwa ikiwemo uanzishwaji wa klabu za lishe mashuleni, kuendeleza stadi za uzalishaji mali, na kuimarisha afya za wanafunzi.
Akihitimisha kikao hicho, Bi. Kalasa amewataka wadau kuendelea kushirikiana na kuongeza juhudi katika kuhimiza matumizi ya lishe bora. Amesema mshikamano huo utasaidia kuongeza kasi ya kupunguza changamoto za lishe na kuimarisha afya ya watoto na Jamii kwa ujumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2025, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.