Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Tanzania inakabiliwa na changamoto ya uhifadhi wa misitu baada ya maeneo mengi kutokuwa na mipaka inayotambulika rasmi.
Kauli hiyo ilitolewa na waziri wa maliasili na utalii, Dr. Hamis Kigwangala alipokuwa akiongea na kamati ya kitaifa ya ushauri wa misitu katika ukumbi wa chuo cha VETA mjini Iringa jana.
Dr. Kigwangala alisema “kwa muda huu mfupi ambao nimekuwepo hapa katika wizara hii, nimegundua kuwa suala la uhifadhi wa misitu ni jambo lenye changamoto nyingi sana. Na changamoto hizi hasa zinatokana na sisi wenye dhamana ya uhifadhi wa misitu hii kwa maana ya watendaji wa taasisi zetu, na hivyo kutoa mwanya kwa misitu yetu mingi kuvamiwa na wananchi” alisema Dr. Kigwangala.
Alisema kuwa wizara yake inaendelea kutekeleza maagizo ya waziri mkuu ya kuweka alama katika misitu yote ili wananchi wapate kuitambua na kuiheshimu. Vilevile, alikemea tabia ya baadhi ya wananchi kugomea zoezi hilo na maeneo mengine kubomoa alama hizo baada ya kuwekwa na wataalamu. Aliwataka wananchi kuheshimu alama hizo ambao ni mkakati wa serikali kumaliza migogoro ya wananchi kuvamia maeneo yaliyohifadhiwa iliyodumu kwa muda mrefu.
Katika salamu za mkuu waa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema kuwa wizara imekuwa ikiunga mkono juhudi za kuendeleza utalii kwa Mkoa wa Iringa na mikoa ya nyanda za juu kusini.
Mkuu wa Mkoa alisema kuwa katika kuhakikisha kuwa utalii unakuwa endelevu, Mkoa wa Iringa umefanya utalii kuwa agenda ya kudumu katika vikao vyake. Alisema kuwa Mkoa umejipanga kuendeleza eneo la Kihesa kilolo kwa kukuza utalii kwa kulitunza, kuliendeleza na kulihifadhi. Utunzaji wa eneo hilo utachangia uendelevu wa sekta ya utalii na uhifadhi mkoani Iringa na ukanda wa nyanda za juu kusini, alisema mkuu wa Mkoa.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.