Tathimini ya Ripoti ya Utafiti wa kimkakati kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Peter Serukamba kuhusu watoto wenye udumavu Mkoa wa Iringa imetolewa leo huku ikionyesha hali ya udumavu kuwa ni asilimia 30.1.
Ripoti hiyo imewasilishwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe ( TFNC) Dkt Germana Levna.
Mnamo tarehe 20 mwezi Machi 2024 Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe Peter Serukamba, alitoa rai kwa viongozi na watendaji kujipanga kutatua KERO za wananchi huku akieleza wazi kukerwa na mfupa wa KERO ya Iringa kuongoza kwa UDUMAVU kwa watoto chini ya miaka 5.
Katika kutekeleza adhima yake kwa vitendo tarehe 10, Julai 2024 alitangaza kuanza kwa siku 4 za KAMPENI MAALUM YA KUTATHIMINI HALI YA LISHE KATIKA MKOA WA IRINGA yenye kauli mbiu “ mtoto kwanza udumavu unazuilika” Tarehe 05 Mwezi Machi 2025 dhamira ya uwazi wa uwajibikaji wa kutatua KERO hii kwa vitendo imedhihirika. Mhe. Serukamba amesema “ anayejua kiatu kinavyobana ni yule aliyekivaa” Baada ya kupokea ripoti hiyo kauli ya Mkuu wa mkoa wa Iringa ni kuongeza nguvu maeneo ambayo yamebainishwa kuwa na changamoto ya udumavu “ mimi na timu yangu tutakaa na kujipanga na kufanyia kazi maeneo ambayo yambainishwa kuwa na changamoto kuanzia ngazi ya Halmashauri, Kata kwa kata/vijiji, hadi Kaya.” amesema Serukamba. Takwimu za udumavu nchini zinaonesha mkoa wa Iringa unaongoza kwa kuwa na asilimia 56.9 ya watoto chini ya miaka mitano wenye udumavu. unafuatiwa na mkoa wa Njombe wenye asilimia 50.4 na Rukwa wenye asilimia 49.8 pamoja na kwamba ripoti ya utafiti wa Hali ya Uzazi ya Afya ya Mama na Mtoto na Maralia inaonesha kuwa hali ya udumavu nchini imepungua hadi asilimia 30 mwaka 2022.
Mwaka 2021, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe Queen C Sendiga alitoa taarifa kwa vyombo vya habari katika wiki la unyonyeshaji akisema, Mkoa wa Iringa una tatizo la udumavu kwa watoto. kwa asilimia 47.1 na kushika nafasi ya tatu kitaifa ukiongozwa na Njombe asilimia 53.6 na wa pili ni Rukwa asilimia 47.9.
Akataja sababu zinazopelekea tatizo hilo la udumavu kuwa ni pamoja na ulevi, kukosekana kwa mabadiliko ya tabia ya ulaji na ulishaji, kuwachelewesha watoto katika matibabu pale watoto wanapougua, kutozingatia kanuni za usafi wa maji, mazingira na chakula, wazazi na walezi kutowekeza muda wa kutosha kuwalisha watoto, wazazi kutowasiliana na watoto katika uchangamshi ikiwemo kucheza na watoto na mazingira wezeshi kwa watoto kucheza.
Kuhusu vikwazo katika unyonyeshaji taarifa hiyo ya Mhe. Sendiga ilisema hali ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa watoto katika miezi sita ya mwanzo ni asilimia 66, na asilimia 12 tu ya watoto wa miezi 6 hadi 23 wanapewa kiasi cha mlo kinachokubalika ( minimum acceptable Diet). Idadi ya milo anayopewa mtoto kupingana na umri (meal frequency ) ni asilimia 23 tu na watoto wanaopewa mlo kamili wenye mchanganyiko wa vyakula vyenye viini Lishe vingi zikiwemo mboga mboga, matunda na vyakula vyenye jamii ya nyama na mikunde ( dietary diversity) ni asilimia 25 tu.Taarifa hiyo iliongeza kuwa katika Mkoa wa Iringa wastani wa asilimia 70 ya watoto walio na umri wa miezi sita Hadi miaka 2 hawalishwi vyakula vya nyongeza vinavyotakiwa.
Kuhusu changamoto kubwa zinazopelekea Mkoa wa Iringa kushindwa kufikia malengo ya Taifa ya kufanikisha ulishaji na kujenga mazingira wezeshi kwa wanawake wanaponyonyesha na kukabili tatizo la udumavu taarifa ilitaja miongoni mwa changamoto hizo kuwa ni pamoja na wazazi walevi kuwapa watoto ulanzi wenye sukari, baadhi ya wanaume kutokua karibu na wenzi wao katika kipindi cha unyonyeshaji, msongo wa mawazo na wasiwasi wanaokumbana nao baadhi ya wanawake zikiwemo kazi nyingi na kukosa muda wa kupumzika na kushindwa kunyonyesha mtoto mara kwa mara nchana na hata usiku, Imani potofu katika jamii juu ya dhana ya kuwa maziwa pekee ya mama pekee hayatoshi kwa mtoto wa chini ya miezi 6 hivyo kupelekea kumpa mtoto uji wenye mchanganyiko wa miti shamba na ulanzi wenye sukari, ulishaji wa vyakula usiozingatia makundi matano kulingana na umri wa mtoto,.
Changamoto nyingine inayobainishwa katika wakati huo ni uwepo waakinamama waliozaa kabla ya kufikia miaka 18 ambapo pia wakina mama hawa wanakosa elimu sahihi ya uzazi na kupelekea kutojali suala la unyonyeshaji, ulishaji na matunzo salama ya mtoto sambamba na kuwalisha watoto chakula chenye nafaka nyingi na kutumia chuchu za mpira kuwapa maziwa watoto na mara nyingine kuwaachia watoto na wazazi au walezi wao ambao ni wazee sana suala linalohatarisha afya na uhai wa mtoto.
Mwaka 2019 Tanzania Home Econimics Association ( TAHEA) kupitia mradi wa “tuwabadilishe” walichapisha taarifa ya tathimini ya matumizi ya pombe kwa akina mama wajawazito na wanaonyonyesha na udumavu kwa watoto, miongoni mwa sababu zilizotajwa kusababisha unywaji huo wa pombe ni pamoja na uvumi, mila na mazoea.
Septemba 2022 Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza kufanyiwa mapitio kwa Sera ya Lishe ya Mwaka 1992, si hivyo tu bali pia aliweka saini Mkataba wa Usimamiaji wa Shughuli za Lishe na mkataba huo huo wakuu wa mikoa walisaini na wakuu wa wilaya na kushusha kwenye ngazi ya Halmashauri hadi Kata/Kijiji ambako utekelezaji wa afua za lishe umekuwa ukitekelezwa kwa ufanisi katika viashiria vyote vya mkataba katika Mkoa wa Iringa
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2025, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.