MKOA WA IRINGA WAZINDUA MPANGO WA USAFI WA MAZINGIRA ENDELEVU
Katika juhudi za kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora na salama za maji na kuishi katika mazingira safi, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, leo Septemba 26, 2025, amezindua mpango mkakati wa uendelevu wa ubora wa usafi wa mazingira mkoani Iringa.
Uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa ambapo Mhe. James amebainisha kuwa mpango huo unalenga kuhakikisha kila mtu anapata huduma bora na salama za maji ifikapo mwaka 2030, sambamba na kuimarisha afya za wananchi na mazingira kwa ujumla.
Aidha, Mhe. James amewataka wakuu wa shule na viongozi wa taasisi mbalimbali kuhakikisha wanadumisha juhudi za kutunza na kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
“Mazingira safi ni msingi wa afya na maendeleo ya jamii. Nawasihi viongozi wote kushirikiana kuhakikisha tunadumisha jitihada hizi kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema Mhe. James.
Mkuu wa Mkoa pia amewapongeza viongozi wa mkoa pamoja na wataalam wa sekta ya afya akisema mchango wao mkubwa ndio umewezesha kufikiwa kwa malengo ya awali katika kuboresha hali ya usafi na upatikanaji wa huduma za maji safi na salama.
Akizungumza na vyombo vya habari, Afisa Afya wa Mkoa wa Iringa, Bi. Khadija Haroun, alisema mpango huo utatekelezwa kuanzia mwaka 2025 hadi 2030. Alifafanua kuwa mkoa wa Iringa tayari umekamilisha hatua ya kuhakikisha kaya zote zinakuwa na vyoo bora, hatua iliyosaidia kufanikisha malengo ya awali katika usafi wa mazingira.
Kwa mujibu wa Bi. Haroun, utekelezaji wa mpango huo unatarajiwa kuongeza ushirikiano wa jamii, taasisi na serikali, ili kuimarisha afya na kulinda mazingira kwa maendeleo endelevu ya mkoa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2025, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.