Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, IRINGA
Manispaa ya Iringa imetakiwa kujenga na kuimarisha vipawa vya wanafunzi kupitia somo la kompyuta ili waweze kuendana na uchumi wa viwanda.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe Ally Hapi alipokuwa akipokea na kukabidhi kompyuta 20 ambazo ni ufadhili wa mbunge wa viti maalum Mkoa wa Iringa, Mhe Rita Kabati leo katika ukumbi wa shule ya sekondari Lugalo.
Mhe Hapi alisema kuwa dunia ya leo inahitaji watu wenye vipawa vingi, miongoni mwa vipawa hivyo ni elimu ya kompyuta. Kompyuta ni moja ya htaji la msingi kumuwezesha binadamu kuishi. “Nipo hapa kwa ajili ya kupokea na kukabidhi kompyuta 20, kati ya hizo, kompyuta 11 ni kwa ajili ya shule za Halmashauri ya Manispaa na zinazobaki kwa ajili ya shule za Halmashauri nyingine katika mkoa wa Iringa. Kompyuta hizi zitoe nafasi kwa wanafunzi wetu kujifunza somo la kompyuta. Dunia ya leo inahitaji watu wenye vipawa vingi ikiwa ni pamoja na kompyuta”. Aidha, alimuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa kuhakikisha kompyuta hizo zinatunzwa na zinatumika vizuri kwa kazi iliyokusudiwa. Kama wataalam wa kufundisha kompyuta ni wachache, wafundishe kwa utaratibu wa mzunguko ili elimu hiyo iwafikie wanafunzi wengi zaidi, alishauri Mhe Hapi.
Wakati huohuo, Mbunge wa viti maalum, Mkoa wa Iringa, Mhe Rita Kabati amepongeza utayari wa Mkuu wa Mkoa wa Iringa katika shughuli za maendeleo na kumuita kuwa ni mzalendo na mtu wa kazi. Aidha, aliongelea tatizo la mawasiliano kupitia minara ya simu katika Mkoa wa Iringa kuwa linawaathiri wanawake zaidi. “Mimi sipendi wanawake wapande kwenye minara kutafuta mtandao. Mkoa wa Iringa bado unahitaji minara ya mawasiliano ya simu. Nitandelea kuwasiliana na mamlaka husika kuhakikisha minara zaidi inajengwa Mkoani Iringa” alisema Mhe Kabati.
Katika hafla ya kupokea na kukabidhi kompyuta 20, Mkuu wa Mkoa alizindua shindando la sayansi kwa shule za Mkoa wa Iringa.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.