Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Viongozi wastaafu katika Mkoa wa Iringa wamepongezwa kwa mafanikio waliyoyapaka katika utumishi wao mkoani hapa.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Ally Hapi alipokuwa akiongea na kamati ya ulinzi na usalama na menejimenti ya mkoa wa Iringa katika hafla ya makabidhiano ya ofisi na mkuu wa mkoa mstaafu Amina Masenza katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa Mkoa.
Hapi alisema “tunawapongeza kwa mafanikio makubwa mliyoyapata katika uongozi wa mkoa wa Iringa. Pongezi kwa mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala Mkoa kwa kazi nzuri mliyoifanya katika maendeleo ya mkoa wa Iringa. Pongezi kwa wakuu wa Wilaya kwa kazi nzuri, mlimpa mkuu wa Mkoa ushirikiano, umoja na upendo katika kutekeleza majukumu yake”.
Akiongelea changamoto katika Mkoa, mkuu wa Mkoa alisema kuwa changamoto ndiyo sababu za kuwepo kwa viongozi. Hivyo, aliwataka viongozi wa serikali kujikita katika kutatua changamoto na kero za wananchi kwa wakati. Alisema kuwa utatuzi wa kero za wananchi kwa wakati unaondoa migogoro na misuguano na kuwapa wananchi muda wa kufanya kazi za maendeleo.
Hapi aliwaomba viongozi wastaafu kutoa ushirikiano kwa viongozi wapya katika kutekeleza majukumu yao. “Ninyi mnauelewa mkubwa katika mkoa huu, pale mnapoona nafasi ya kutushauri, kutupa taarifa msisite kufanya hivyo. Tunatarajia busara yenu na mawazo yenu katika kufikia mafanikio ya Mkoa wetu wa Iringa” alisema Hapi.
Awali mkuu wa mkoa mstaafu, Amina Masenza alisema kuwa hali ya ulinzi na usalama inaendelea kuimarika katika Mkoa wa Iringa kwa kushirikisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama na wananchi kwa ujumla. Kutokana na hali ya usalama kuwa nzuri, wananchi wanaendelea kutekeleza majukumu yao vizuri, aliongeza. Hali ya siasa ni nzuri, na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM unaendelea vizuri.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.