Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza ameridhishwa na hali ya maandalizi ya mabanda ya maonesho ya shughuli na huduma zinazofanywa na wafanyazi nchini.
Akitoa hali ya tathmini ya mabanda ya maonesho baada ya kuyatembelea jana jioni mbele ya waandishi wa habari katika uwanja wa maonesho wa Kichangani, Masenza alisema kuwa ameridhishwa na hali ya mabanda. “Hadi sasa mabanda yamekwisha pambwa vizuri na huduma na bidhaa mbalimbali zimeanza kuoneshwa mezani na wananchi wakitembelea mabanda hayo makumi kwa mamia”. Aidha, alitoa rai kwa wajasiriamali wa mkoa wa Iringa kuendelea kujitokeza kuonesha bidhaa zao kwa sababu nafasi za mabanda bado zipo. Alisema maonesho ya bidhaa na huduma za wanafanyakazi ni fursa nzuri kujitangaza na kutangaza huduma na bidhaa zinazofanywa na wafanyakazi ndani na nje ya mkoa.
Mkuu wa mkoa amewataka wananchi wote katika Manispaa ya Iringa na vitongoji vyake kujitokeza kwa wingi kutembelea mabanda na kujionea bidhaa na huduma zinazooneshwa pamoja na kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu masuala afya na usalama mahala pa kazi. Alisema kuwa maonesho hayo yatafunguliwa rasmi tarehe 27/4/2-18.
Awali mkuu wa mkoa alitembelea uwanja wa michezo wa Samora kuangalia ukarabati kwa ajili ya maadhimisho ya sherehe za Mei Mosi, 2018.
Mkoa wa Iringa ni mwenyeji wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi (Mei Mosi) kitaifa na mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.