Zaidi ya washiriki 10,000 wanatarajiwa kushiriki mashindano ya kitaifa ya michezo kwa shule za msingi na sekondari, UMITASHUMTA na UMISSETA, yatakayofanyika mkoani Iringa kwa mara ya kwanza mwaka 2025, tukio linalotajwa kuwa la kihistoria kwa Mkoa wa Iringa .
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Peter Serukamba, amethibitisha hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa mashindano hayo ni fursa adhimu kwa mkoa wa Iringa, huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuiamini Iringa kuwa mwenyeji wa tukio hilo la kitaifa.
“Tunamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia kwa kutupatia heshima hii kubwa, Kwa mara ya kwanza Iringa itakuwa mwenyeji wa mashindano haya makubwa, baada ya kuwa yamefanyika mkoani Tabora kwa mfululizo Kwa miaka mitatu ,” amesema Mhe. Serukamba.
Kwa mujibu wa ratiba rasmi, mashindano ya UMITASHUMTA yataanza tarehe 08 Juni hadi 17 Juni 2025, yakifuatiwa na mashindano ya UMISSETA yatakayodumu kuanzia tarehe 08 hadi 30 Juni 2025.
Mashindano hayo yanatarajiwa kukutanisha wanafunzi, walimu wa michezo, maafisa pamoja na viongozi mbalimbali kutoka sekta ya elimu na michezo kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani.
Michezo itakayoshindaniwa ni pamoja na mpira wa miguu, mpira wa kikapu, mpira wa wavu, netiboli, pamoja na mchezo wa kengele kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum. Aidha, burudani ya muziki wa kizazi kipya pia itakuwepo, ikitumbuiza na kuhamasisha washiriki na mashabiki.
Viwanja vitakavyotumika katika mashindano hayo ni pamoja na Shule ya Sekondari Wasichana Iringa, Shule ya Sekondari Lugalo, pamoja na Chuo cha Ualimu Klerru.
Aidha Mhe. Serukamba amewataka wananchi wa Iringa kutumia vyema fursa hii kwa kutoa huduma mbalimbali zitakazowawezesha kunufaika kiuchumi.
“Wananchi wanayo nafasi ya kipekee ya kunufaika na wageni watakaofika hapa. Huduma za malazi, vyakula, usafiri na biashara ndogondogo zote zitahitajika.
Ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia ufunguzi rasmi wa mashindano hayo utakaofanyika tarehe 09 Juni 2025
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2025, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.