WATUMISHI WANAOSHIRIKI MCHEZO WA MPIRA WA MIGUU MKOANI IRINGA WATAKIWA KUCHEZA KWA NIDHAMU
Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Watumishi wa taasisi mbalimbali mkoani Iringa wametakiwa kucheza kwa nidhamu na kuepuka ugomvi katika mashindano ya mpira wa miguu yanayoendelea mkoani Iringa.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hotuba yake ya ufunguzi wa mchezo wa mpira wa miguu kwa taasisi za mkoa wa Iringa iliyosomwa kwa niaba yake na mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela katika uwanja wa chuo cha ualimu Kleruu kilichopo Manispaa ya Iringa leo.
Masenza aliwataka wachezaji hao kucheza kwa nidhamu na kuepuka kuchochea ugovi. Alisema kuwa mchezo wa mpira wa miguu ni burudani na unajenga urafiki hivyo, mashindano hayo yatumike kutoa burudani na kujenga urafiki miongoni mwa wanamichezo hao. Aliongeza kuwa mashindano hayo yatumike kujenga uzalendo kwa watumishi wa umma na watumishi wa taasisi zisizo za kiserikali mkoani Iringa. Aidha, aliwataka wanamichezo hao kutengeneza mtandao utakaowaunganisha kama wanamichezo na watumishi wa taasisi mbalimbali.
Katika salamu za afisa michezo Mkoa wa Iringa, Kenneth Komba kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, alisema kuwa michezo hiyo ni wazo la mkuu wa Mkoa wa Iringa kutaka kuwaunganisha watumishi wa taasisi za Mkoa wa Iringa kupitia mchezo wa mpira wa miguu. Alisema kuwa hadi kufikia jana jumla ya taasisi 21 zilikuwa zimejitokeza kushiriki mashindano hayo.
Wakati huohuo, mechi ya ufunguzi, timu ya Timu ya RAS Iringa ilikubali kichapo cha magoli 5 bila kutoka TANROADS.
Mashindano ya mpira wa miguu kwa taasisi za Mkoa wa Iringa ni mashindanao ya kwanza ya aina yake kufanyika mkoani hapa yakikabiliwa na changamoto ya udhanimi.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Anuani ya Posta: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Simu: +255 262 702 715
Mobile:
Barua pepe: ras@iringa.go.tz
Hakimiliki ©2024, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa.