Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Benki ya MUCOBA kutoa fursa ya mikopo ya stakabadhi ghalani ili kuwanufaisha wakulima wa mpunga wilayani Iringa.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hotuba yake ya uzinduzi wa mfumo wa mikopo ya stakabadhi ghalani kupitia benki ya MUCOBA katika Tarafa ya Pawaga, wilayani Iringa.
Masenza alisema kuwa wakulima wamekuwa na changamoto ya upatikanaji bei nzuri ya mpunga katika Tarafa ya Pawaga. “Jambo hili limesababisha wakulima wetu kuendelea kunyonywa na walanguzi kwa kuuza mazao yao kwa bei ya chini na kusababisha wakulima wa Mkoa wa Iringa na Tanzania kwa ujumla kuendelea kuwa masikini na huku walanguzi wakiendelea kuneemeka zaidi kwa jasho la wakulima wetu. Hivyo basi, kwa uamuzi huu wa Benki ya MUCOBA wa kuweza kuanzisha fursa hii ya mikopo ya stakabadhi ghalani ili wakulima wetu waweze kutunza mazao yao katika Ghala hili na kupewa mikopo ya riba nafuu, ili kusaidia wakulima kujikimu wakati wakisubiria soko na bei nzuri za mazao yao” alisema Masenza. Benki ya MUCOBA ni ukombozi kwa wakulima wa mpunga katika Tarafa ya Pawaga, alisema. Aidha, aliwataka wakulima wa mpunga wa Pawaga kuchangamkia fursa hiyo muhimu na kuunga mkono juhudi za benki na serikali.
Mkuu wa Mkoa alitoa wito kwa wadau kushirikiana na benki ya MUCOBA kutoa elimu na kuwahamasisha wananchi kutumia fursa ya mikopo ya stakabadhi ghalani. “Ninatambua ukweli kuwa wakulima wengi hawana elimu ya kutosha kuhusu stakabadhi ghalani, hivyo napenda kutoa wito kwa wadau wengine wote kushirikiana na Benki ya MUCOBA kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kutumia fursa hii ya mikopo ya stakabadhi ghalani na pia kutumia huduma bora za benki ya MUCOBA hapa Pawaga na maeneo mengineyo ambako Benki inafanya shughuli zake. Pia sisi kama serikali tutakuwa bega kwa bega katika kusaidia juhudi za kuwaelimisha wakulima wetu juu ya umuhimu wa stakabadhi ghalani, pia hatuta sita kusaidiana na Benki yetu ya wananchi MUCOBA kupeleka huduma hii mahali pengine” alisema Masenza.
Benki ya MUCOBA imefungua kituo cha huduma za kifedha katika Tarafa ya Pawaga ili kuweza kuwahudumia wananchi wanyonge kupata mikopo kwa ajili ya kilimo cha mpunga wilayani Iringa.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.