DKT. SAMIA AIBADILISHA IRINGA KWA Bil. 7.5 ZA ELIMU – RC KHERI ATOA SHUKRANI
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri James, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuupatia Mkoa huu kiasi cha Shilingi bilioni 7.5 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu ya awali na msingi kupitia Programu ya BOOST.
Mhe. Kheri ametoa shukrani hizo leo, Agosti 4, 2025, katika kikao maalum kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, kilichowakutanisha Maafisa Elimu, Maafisa Manunuzi na Wahandisi kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Iringa, kwa lengo la kujadili utekelezaji wa miradi hiyo ya elimu.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe.Kheri amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha kuwa matumizi ya fedha hizo yanaendana ipasavyo na thamani ya miradi inayoendelea kutekelezwa. Aidha, amesisitiza uwajibikaji, ufuatiliaji wa karibu, na matumizi bora ya fedha za umma ili kuleta tija na kuboresha mazingira ya ujifunzaji kwa watoto.
"Ni lazima tuhakikishe fedha hii ya Serikali inaleta matokeo yaliyokusudiwa. Miundombinu bora ya elimu ndiyo msingi wa kuandaa kizazi bora cha baadaye,"
Akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo, Afisa Elimu wa Mkoa wa Iringa, Bi. Marry Lyimo, amesema kuwa mwishoni mwa mwaka wa fedha 2024/2025, Mkoa wa Iringa umepokea jumla ya Shilingi bilioni 7.5 kupitia Programu ya BOOST. Kati ya fedha hizo, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imepokea Shilingi bilioni 1.4, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa bilioni 2.0, Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo bilioni 2.2, Halmashauri ya Mji wa Mafinga milioni 512, na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi bilioni 1.3
Pia Bi. Lyimo Akabainisha kuwa jumla ya shule 47 zinanufaika na fedha hizo kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu.
Programu ya BOOST inalenga kuboresha elimu ya awali na msingi nchini kwa kujenga na kukarabati madarasa, ofisi za walimu, matundu ya vyoo, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama katika shule.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.