Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Mkoa wa Iringa umeshika nafasi ya nne kitaifa katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka 2017 kati ya mikoa 26 ya Tanzania bara.
Kauli hiyo ilitolewa na kaimu afisa elimu Mkoa wa Iringa, Mwl Farida Mwasumilwe alipokuwa akisoma taarifa ya maadhimisho ya wiki ya kusoma mkoani Iringa yaliyofanyika katika mji mdogo wa Ilula wilayani Kilolo.
Mwl Mwasumilwe alisema kuwa Mkoa wa Iringa ni miongoni mwa mikoa inayofanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba. “Kwa mtihani uliofanyika mwezi Septemba, 2017 Mkoa umeshika nafasi ya 4 kati ya Mikoa 26 ya Tanzania Bara ukiwa na ufaulu wa asilimia 83.14 ambapo jumla ya wanafunzi 20,606 wamechaguliwa na kujiunga na kidato cha kwanza 2018. Aliongeza kuwa ufaulu wa mwaka 2015 Mkoa ulikuwa nafasi ya 10 ukiwa na ufaulu wa asilimia 73.25. Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na Wilaya ya Kilolo ufaulu umekuwa ukiongezeka kuanzia mwaka 2015-2017” alisema Mwl Mwasumilwe.
Akiongelea shule 10 zilizofanya vizuri ngazi ya Mkoa, Mwl Mwasumilwe alisema kuwa Mkoa ulikuwa na shule 481 zilizofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.
Katika shule 10 zilizofanya vizuri kimkoa, shule tatu ni za serikali na saba ni binafsi, alisema. Alizitaja shule hizo kuwa ni Sipto (Manispaa), St Dominic Savio (Manispaa), Star (Manispaa), Ukombozi (Manispaa), BrookeBond (Mufindi), Ummusalama (Manispaa), Lukwambe (Iringa DC), St Charles (Manispaa), Southern Highlands (Mji Mafinga) na Nyamalala (Mji Mafinga)
Maadhimisho ya wiki ya kusoma mkoani Iringa yaliongozwa na kaulimbiu isemayo “Stadi za kusoma, kuandika, na kuhesabu ni msingi wa elimu; tuwekeze katika elimu kuelekea uchumi wa viwanda”.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.