Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Mkoa wa Iringa umeshika nafasi ya nne kati ya mikoa 26 katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba kwa mtihani uliofanyika mwaka 2017.
Kauli hiyo ilitolewa na afisa elimu taaluma Mkoa wa Iringa, Mwalimu Farida Mwasumilwe alipokuwa akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya sekta ya elimu Mkoa wa Iringa katika kikao cha wadau wa elimu Wilaya ya Kilolo, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya Wilaya ya Kilolo.
Mwalimu Mwasumilwe alisema kuwa Mkoa wa Iringa umekuwa ukifanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa kumaliza darasa la saba kwa miaka kadhaa. “Kwa mtihani uliofanyika mwezi Septemba, 2017 Mkoa umeshika nafasi ya nne kati ya mikoa 26 ya Tanzania bara ukiwa na ufaulu wa asilimia 83.14 ambapo jumla ya wanafunzi 20,606 wamechaguliwa na kujiunga na kidato cha kwanza 2018, ukilinganisha na ufaulu wa mwaka 2015 ambapo mkoa ulikuwa nafasi ya 10 ukiwa na ufaulu wa asilimia 73.25” alisema Mwalimu Mwasumilwe. Ufaulu umekuwa ukiongezeka kwa halmashauri ya Manispaa ya Iringa na halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, aliongeza.
Akiongelea, hali ya miundombinu na samani katika shule za msingi, afisa elimu taaluma mkoa alisema kuwa mkoa una vyumba vya madarasa 4,153, nyumba za walimu 2,203 matundu ya vyoo 7,283 na madawati 99,386. Mkoa umeendelea kuhakikisha miundombinu muhimu na samani vinapatikana katika shule ili kuboresha mazingira ya utoaji elimu, aliongeza.
Akiongelea mikakati ya kukabiliana na upungufu wa miundombinu, afisa elimu taaluma huyo alisema kuwa mkoa umeendelea kutenga fedha kupitia halmashauri zake kutoka katika mapato ya ndani, ruzuku ya serikali na kuwashirikisha wadau wa maendeleo kuchangia ujenzi wa miundombinu ya elimu katika shule za msingi.
Mkoa wa Iringa una jumla ya shule za msingi 499, zikiwa ni ongezeko la asilimia 3.1 mwaka 2018 ikilinganishwa na idadi ya shule 484 mwaka 2015.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.