Redio za ndani ya Mikoa zimetakiwa kujikita katika kutoa huduma ya habari za vijijini ili wananchi hao wanufaike na huduma hizo.
Kauli hiyo ilitolewa na mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Iringa ambaye ni Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akikagua banda la kituo cha redio cha Big Star katika uwanja wa maonesho ya Nanenane wa John Mwakangale mjini Mbeya.
Wamoja alisema kuwa redio za ndani zinawajabu wa kutoa huduma za habari zaidi vijijini. Aliongeza kuwa vituo vingi vya redio vipo katika makao makuu ya miji na masafa yake kuishia katika miji. “Local redio toeni huduma za habari za wananchi walio vijijini kwa sababu wanakosa fursa za kupata habari. Wananchi walio katika miji wana nafuu kwasababu redio nyingi zinapatikana mjini na vyombo vingine vya habari vinapatikana huko kama televisheni” alisisitiza Ayubu.
Aidha, alivitaka vituo vya redio kuwaalika viongozi wa umma katika redio kusikiliza kero za wananchi na kujibu hoja na maswali ya wananchi katika kuboresha utawala bora. Aliongeza kuwa vituo vya redio vitapotenga muda kwa ajili ya viongozi kusikiliza kero za wananchi kutasaidia katika utatuzi wa kero na kuwawezesha wananchi kuchapa kazi katika mazingira mazuri na rafiki. “Endeleeni kuhabarisha wananchi kwa sababu wananchi wanawategemea na kuwahitaji zaidi” alisisitiza Ayubu.
Kituo cha redio cha Big Star kilianza kurusha matangazo yake mwaka 2015 mjini Mbeya katika masafa ya 106.3 MHz kwa sasa redio hiyo inasikika katika mikoa ya Mbeya na Songwe, na baadhi ya maeneo ya mikoa ya Rukwa, Katavi, Njombe, Iringa na Ruvuma.
Maonesho ya shughuli za wakalima Nanenane mwaka 2017 yanaongozwa na kauli mbiu isemayo, “zalisha kwa tija mazao na bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi kufikia uchumi wa kati”.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.