Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkoa wa Iringa umefanikiwa kuongeza pato lake hadi kufikia zaidi ya shilingi trilioni tano mwaka 2016 na kuufanya kuwa Mkoa wa tano kwa kigezo cha GDP kitaifa.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akiwasilisha taarifa fupi ya Mkoa wa Iringa kwa wajumbe kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania waliofanya ziara ya mafunzo ya siku tano mkoani Iringa katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa Mkoa.
Masenza alisema “pato la Mkoa wa Iringa (GDP) limeongezeka kutoka shilingi trilioni 2.3 mwaka 2010 hadi kufikia shilingi trilioni 5.10 Mwaka 2016, wakati pato la mkazi [Per Capita GDP) mwaka 2010 lilikuwa shilingi 1,330,118 ambalo limeongezeka hadi kufikia shilingi 2,982,569 mwaka 2016”. Aliongeza kuwa takwimu hizo za (GDP) kwa mwaka 2016, Mkoa wa Iringa umekuwa ni Mkoa wa tano kwa ngazi ya GDP kitaifa na Mkoa wa tatu kwa pato la mkazi ukitanguliwa na Mkoa wa Dar es Salaam na Mbeya. Aliongeza kuwa pato la Mkoa huchangiwa kwa kiasi kikubwa na mashamba makubwa ya chai, viwanda vya chai, misitu, viwanda vya mbao na tumbaku.
Akiongelea shughuli za kiuchumi, mkuu wa Mkoa alizitaja kuwa ni kilimo, ufugaji, upasuaji mbao, uvuvi, biashara, ajira za ofisini na viwandani. “Asilimia 75 ya wakazi wa Mkoa huu hujishughulisha zaidi na Kilimo pamoja na ufugaji. Mazao ya kilimo yanayolimwa katika Mkoa huu ni mahindi, maharage, mpunga, ngano, viazi, pareto, chai, matunda, alizeti, karanga, ufuta, nyanya, vitunguu, tumbaku, soya na mtama” alisema Masenza.
Nae kiongozi wa msafara wa wajumbe kutoka Chuo cha Ulinzi cha Taifa, Kapten Msafiri Hamisi alipongeza juhudi zinazofanywa na serikali ya Mkoa katika kuwahudumia wananchi. Aidha, alishukuru mapokezi waliyopewa na uongozi wa Mkoa na kuomba ushirikiano huo uwe undelevu.
Kwa matokeo ya Sensa ya mwaka 2012 Mkoa wa Iringa ulikuwa na watu 941,238 kati ya hao wanaume walikuwa 452,052 na wanawake 489,186 na wastani wa ongezeko la idadi ya watu kwa mwaka ni asilimia 1.1. Makadirio ya idadi ya watu kwa mwaka 2017 ni watu 1,000,040; wanaume wakiwa 480,293 na wanawake 519,747.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.