Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wanafunzi wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini (TASAF) wametakiwa kusoma kwa juhudi na maarifa na kuacha utukutu ili wawe raia wenye mchango kwa Taifa lao.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipofanya ziara ya kutembelea wanufaika wa TASAF kupitia elimu katika Manispaa ya Iringa.
Ayubu alisema “serikali tunategemea msome kwa bidii sana na msiwe watukutu. Nia ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dr. John Magufuli ni kujenga msingi imara kwa wananchi wake kupitia elimu. Tunataka kuwa na Taifa lenye wananchi wenye uwezo wa kufanya kazi na kujitegemea”. Alisema kuwa wanafunzi hao wamepata fursa ya kupata elimu bila malipo na fedha kupitia TASAF kwa ajili ya kununua mahitaji muhimu ya shule.
Katibu Tawala Mkoa, alisema kuwa wapo wazazi wanaozembea kuwanunulia watoto wao wanufaika wa TASAF wafuatiliwe ili waweze kutimiza wajibu huo. Alisema kuwa lengo la fedha hizo ni kuwawezesha watoto hao kupata sare za shule, madaftari, kalamu na mahitaji mengine muhimu ya shule. “Hapa lazima ifahamike kuwa, fedha hizi si za wazazi wla walezi, ni fedha kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wanufaika kupata mahitaji yao ya lazima kwa ajili ya shule ili wasijisikie wanyonge pindi wanapokuwa shuleni” alisisitiza Ayubu.
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa alifanya ziara maalum ya ufuatiliaji kwa wanafunzi wanufaika wa mpango wa TASAF kupitia elimu katika Manispaa ya Iringa kujifunza changamoto zinazowakabili. Katika ziara hiyo aliambatana na mratibu wa TASAF Mkoa, afisa mipango, mhasibu, mkaguzi wa ndani na afisa habari.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.