Na. Dennis Gondwe, Afisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-IRINGA
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe Ally Hapi ameridishwa na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM katika ujenzi na ukarabati wa shule ya sekondari ya ufundi ya Ifunda uliotumia zaidi ya shilingi bilioni tatu.
Mhe Hapi alisema hayo baada ya kukagua ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule ya sekondari ya ufundi ya Ifunda na kuongea na jumuiya ya wanafunzi na wafanyakazi wa shule hiyo leo. “Nimefurahi kuona kazi za utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM katika kukarabati shule kongwe nchini. Serikali ilifanya juhudi za kuziokoa shule kongwe ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira mazuri” alisisitiza Mhe Hapi.
Mkuu wa mkoa alisema kuwa ujenzi na ukarabati wa shule hiyo umelenga kuwawekea mazingira mazuri ya walimu ya kufundishia na wanafunzi kujisomea. “Ndugu zangu ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika shule hii unalenga pia kuondoa mirorogo na migomo kutokana na ubovu na uchakavu wa miundombinu. Tunamshukuru Mhe Rais kwa kuamua kukarabati shule hii. Hapa pekee serikali imeleta shilingi Bilioni 3.6. ni fedha inayoweza kujenga vituo 9 vya afya. Serikali imeamua fedha zote ziletwe hapa, wanafunzi na walimu mnatakiwa kujivunia jambo hili” alisema Mhe Hapi.
Aliwataka walimu na wanafunzi kutunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu na kunufaisha vizazi vijavyo.
Katika taarifa ya ukarabati mkubwa katika shule ya sekondari ya ufundi Ifunda kwa programu ya lipa kulingana na matokeo iliyosomwa na mkuu wa shule hiyo Mwl Yusuph Mwagala, alisema kuwa wizara yenye dhamana na elimu iliingia mkataba na chuo kikuu cha Sayansi na Teknolojia–Mbeya kuwa msimamizi mshauri wa mradi wa ukarabati wa miundombinu katika shule ya sekondari ya ufundi Ifunda. “Ukarabati huo ulilenga kuboresha miundombinu ya mabweni, madarasa, matundu ya vyoo, karakana za ufundi, vyumba vya maabara, ukumbi wa mikutano, mabwalo ya kulia chakula, jiko, ofisi ya walimu, jingo la utawala, maktaba, mfumo wa umeme na mfumo wa maji safi na taka. Gharama ya mradi huo ni shilingi 3,609,199,839” alisema Mwl Mwagala.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.