Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, IRINGA
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe Ally Hapi kujenga kituo cha kuibua vipaji vya sayansi na teknolojia ili kuibua na kuchochea ubunifu kwa vijana mkoani hapa.
Kauli hiyo aliitoa katika hafla fupi ya kupokea na kukabidhi kompyuta 20 ambazo ni ufadhili wa mbunge wa viti maalum Mkoa wa Iringa, Mhe Rita Kabati katika ukumbi wa shule ya sekondari Lugalo leo.
Mhe Hapi alisema “nafikiria kuanzisha kituo cha kuibua na kukuza vipaji vya sayansi, teknolojia na ubunifu kwa vijana katika Mkoa wa Iringa. Kituo hiki nataka kiwe na kompyuta za kutosha na mtandao wa intaneti wa bure ili vijana waje wabuni mawazo yao na kuyaendeleza katika kituo hicho”. Alisema kuwa katika kituo hicho, shirika la kuhudumia viwanda vidogo, mamlaka ya mawasiliano Tanzania na wadau wengine wanaohusika na uibuaji na ukuzaji wa sayansi na teknolojia watashirikishwa.
Mkuu wa Mkoa aliahidi kuendelea kuwaunga mkono wale wote wenye nia ya kuleta maendeleo katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa. “Ndugu zangu, tusikate tama, tusonge mbele katika kutatua kero za wananchi na kuwaletea maendeleo” alisisitiza Mhe Hapi.
Wakati huohuo, Mbunge wa viti maalum, Mkoa wa Iringa, Mhe Rita Kabati, aliishukuru Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kudhamini shindano la masomo ya sayansi kwa shule za sekondari Mkoa wa Iringa zinazofundisha masomo ya sayansi. Alisema kuwa nchi inapoelekea katika uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025, lazima vijana waandaliwe katika masomo ya sayansi na ufundi. Aliongelea changamoto ya upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi na maabara katika Mkoa wa Iringa kuwa ni jambo linalohitaji nguvu ya pamoja.
Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Iringa amewezesha upatikanaji wa kompyuta 20, kati ya hizo, 11 kwa ajili ya Manispaa ya Iringa na tisa kwa ajili ya shule za Halmashauri za wilaya za Mkoa wa Iringa.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.