Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Serikali imeandaa mkakati wa kuendeleza biashara ndogo kwa lengo la kufikia uchumi unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akifungua maonesho ya wajasiriamali wadogo na wa kati katika uwanja wa mashujaa mjini Mafinga jana.
Masenza alisema kuwa katika nchini nyingi duniani, asilimia kubwa ya pato la watu binafsi linatokana na biashara ndogo na za kati. “Hivyo kuendeleza sekta hii ni mkakati wa kutimiza malengo ya dira ya maendeleo ya Taifa ni kuwa na uchumi imara unaotegemea uzalishaji katika viwanda ifikapo 2025” alisema Masenza. Aidha, aliwataka SIDO kuandaa mkakati wa kuwasaidia wajasiriamali waweze kupata masoko ya kudumu ndani na nje ya nchi.
Akiongelea changamoto ya uingizaji bidhaa kutoka nje, mkuu wa mkoa alisema kuwa uzalishaji wa bidhaa nyingi ndiyo suluhisho la kujitegemea kwa mkoa wa Iringa. Alisema kuwa uzalishaji huo utapunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi na kuongeza matumizi ya malighafi zinazozalishwa ndani kutumika katika viwanda vya ndani. “Utaratibu huu utasaidia kulinda viwanda vyetu wenyewe bila kutegemea masoko ya nje tu kwa baadhi ya malighafi zetu” alisema mkuu wa mkoa.
“Katika kipindi hiki chenye changamoto za kiuchumi duniani tujitahidi kuzalisha bidhaa kwa wingi na zenye ubora wa hali ya juu ili kuongeza ajira na pato la Taifa. Wananchi wote, wafanyabiashara na viongozi mliobahatika kutembelea maonesho haya, hii ni fursa nzuri ya kuweka miadi na kununua au kuchangia mawazo yenu katika kuboresha bidhaa zetu za hapa nchini, ili kusaidia kujenge msingi imara wa viwanda na uchumi wetu” alisisitiza mkuu wa mkoa.
Maonesho ya wajasiriamali kwa mkoa wa Iringa ni ya kwanza ya aina yake yaliyoandaliwa na T-LED, SIDO, TCCIA, TWCC kwa kushirikiana na Halmashauri ya mji wa Mafinga.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.