Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Serikali inahitaji takwimu sahihi ili kuweza kupanga mipango ya maendeleo kwa ustawi wa wananchi wake.
Kauli hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akipokea vifaa vya TEHAMA na samani kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya elimu, sayansi na teknolojia katika viunga vya Ofisi ya mkuu wa Mkoa jana.
Masenza alisema kuwa takwimu sahihi ni muhimu katika kuiwezesha serikali kupanga mipango katika ustawi wa jamii. “Takwimu sahihi ni muhimu sana katika kuiwezesha serikali kuweka mipango mbalimbali kwa ajili ya ustawi wa jamii katika huduma za elimu, afya, maji na mgawanyo wa maliasili tulizonazo kwa uwiano unaotakiwa. Kiujumla takwimu sahihi ni kila kitu katika kupanga maendeleo ya watu na shughuli zao” alisema Masenza.
“Ndugu waandishi wa habari, nimewaita hapa kushuhudia kupokea vifaa vya TEHAMA na samani. Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kushirikiana na wizara ya elimu, sayansi na teknolojia imenunua vifaa vya TEHAMA (seti ya komputa, printa na UPS, viti na meza) kwa ajili ya kuboresha zoezi la uandaaji na uingizaji wa takwimu za elimu msingi” alisema Masenza. Takwimu hizo zitaingizwa kupitia mfumo wa ‘basic education management information system’-BEMIS.
Vifaa hivyo vitafungwa katikamofisi za maafisa elimu vifaa na takwimu kwa halmashauri zote nchini na maafisa elimu taaluma kwa ngazi za mikoa. Aidha, mkoa na halmashauri zimepatiwa komputa tatu, printa moja na UPS tatu pamoja na meza tatu na viti vitatu.
Ikumbukwe kuwa vifaa hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa GPE-LANES.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.