Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Vyombo vya habari mkoani Iringa vimetakiwa kuhamasisha jamii ili wasichana wenye umri wa miaka 14 waweze kuchanjwa kujikinga na saratani ya mlango wa kizazi inayoua wanawake wengi nchini.
Ombi hilo lilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akiongea na wahariri, mameneja vipindi na watangazaji wa redio za mkoa wa Iringa kuhusu nafasi yao katika kuhamasisha jamii juu ya chanjo mpya ya saratani ya mlango wa kizazi inayoanza kutekelezwa mkoani Iringa. Kikao hicho cha elimu na hamasa kilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo kikuu hurua mjini Iring.
Masenza alisema kuwa vyombo vya habari hasa redio vinanafasi kubwa ya kusaidia kufikisha elimu na hamasa kwa jamii juu ya kampeni zinazofanywa na serikali.
“Ombi kubwa la serikali ni kuwaomba wanahabari wote mliopo hapa mtusaidie kupeleka ujumbe huu wa kuanzishwa kwa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa mabinti wa miaka 14 ili waweze kukingwa na madhara makubwa yanayoweza kuwapata hapo baadae ya kuugua kwa maumivu makali sana na hatimaye kifo. Wengi wetu tumetembelea Ocean Road na kuona jinsi jamaa zetu wanavyopata mateso makali” alisema Masenza.
Mkuu wa mkoa aliwashukuru wadau waliochangia katika kufanikisha utoaji bora wahuduma za chanjo hapa nchini.
“Natoa shukurani zangu za dhati kabisa kwa shirika la GAVI, Shirika la afya ulimwenguni WHO, Shirika la kuhudumia watoto UNICEF, CHAI, JSI, PATH, AMREF, JHPIEGO pamoja na wadau wengine kwa misaada yao ambayo imeweza kutufikisha hapo” alisema Masenza.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.