Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa- Iringa
Serikali ya Mkoa wa Iringa imewanyooshea kidole watumishi wanaogeuza fedha za miradi ya maendeleo kuwa sehemu ya kujinufaisha wenyewe tofauti na madhumini ya fedha hizo.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe Ally Hapi alipokuwa akiongea na wananchi wa Tarafa ya Sadani wilayani Mufindi leo katika siku yake ya nne ya ziara ya Tarafa kwa Tarafa wilayani Mufindi.
Mhe Hapi alisema “Serikali ya awamu ya tano inaleta fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi. Wapo baadhi ya watendaji wanazigeuza fedha za Serikali kama shamba la bibi. Nimekuja kuhakikisha tunasimamia vizuri miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za Serikali. Leo nipo Tarafa ya nne tangu nimeanza ziara ya kutembelea Tarafa kwa Tarafa ambapo miradi mitatu nimeshawakabidhi TAKUKURU washughulike nayo kutokana na kutoridhika na jinsi fedha ya Serikali ilivyotumika” alisema Mhe Hapi.
Mkuu wa Mkoa alisema kuwa amekuja Iringa kuhakikisha miradi ya maji inatekelezwa vizuri na hakuna mchwa wanaotafuna fedha za Serikali katika miradi hiyo. “Tunafahamu kuwa yapo matatizo ya pembejeo kuchelewa, pembejeo kuuzwa kwa gharama kubwa kuliko bei elekezi za Serikali tunayatafutia ufumbuzi” alisema Mhe Hapi. Lengo la serikali ni kuona wakulima wananufaika na kilimo na kujiletea maendeleo, aliongeza.
Mkuu wa Mkoa aliwaasa watendaji wanaowanyanyasa wananchi. “Wapo baadhi ya watendaji ambao ni vinara wa kunyanyasa wananchi, mwenye pesa anapewa haki masikini ananyimwa haki. Kiongozi na mtendaji ambaye hatatui kero za wananchi hatufai. Hii ni nchi yetu sote, lazima tulinde rasilimali za nchi yetu na watu wake. Asiyeweza kwendana na kasi yangu aandike barua aache kazi akatafute kazi nyingine” alisema Mhe Hapi.
Akiwa katika Tarafa ya Sadani Mkuu wa Mkoa alikagua ujenzi wa tanki la maji kijiji cha Maduma, kukagua ufugaji wa nyuki, alikagua lambo la mifugo na shamba la matikiti maji la mwananchi. Shughuli nyingi alizofanya ni kukagua ujenzi wa hosteli ya sekondari Mgalo na kufanya mkutano na wananchi wa Tarafa ya Sadani na kusikiliza kero za wananchi.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.