Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Wanafunzi nchini wametakiwa kusoma kwa bidii ili kuunga mkono uwekezaji wa serikali katika sekta ya elimu ili ichangie katika uchumi wa viwanda.
Kauli hiyo iliyolewa na kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2018, Charles Kabeho alipokuwa akitoa ujumbe wa Mwenge wa uhuru katika sekondari ya Igombavanu wilayani Mufindi leo.
Kabeho alisema kuwa serikali inayoongozwa na Rais, Dkt John Magufuli imeondoa ada na michango shuleni ambayo ilikuwa ni kero kwa wananchi ili wanafunzi wengi waweze kufurahia haki ya kupata elimu nchini. Alisema kuwa elimu ni muhimu sana kwa jamii katika utekelezaji wa dhamira ya serikali ya kuelekea uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025. “Uchumi wa viwanda unategea sana uwekezaji katika elimu. Serikali ya awamu ya tano kwa kuona umuhimu huo, iliamua kutoa elimu bila malipo ili watanzania wote wapate elimu hiyo msingi” alisema Kabeho. Aidha, aliongeza kuwa serikali imedhamiria kuboresha elimu kuanzia ya awali hadi elimu ya juu. Uboreshaji wa sekta ya elimu nchini unakwenda pamoja na ukuaji wa elimu ya ufundi na ufundi stadi kwa kuweka msisitizo katika maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu, aliongeza.
Mwenge wa uhuru mwaka 2018, ukiwa wilayani Mufindi utatembelea miradi sita ya maendeleo yenye thamani ya shilingi 9,199,229,136. Kati ya fedha hizo mchango wa serikali kuu shilingi 55,700,000. Halmashauri shilingi 97,933,250, wadau wa maendeleo shilingi 8,976,015,936 na nguvu za wananchi shilingi 69,579,950.
=30=
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, 4 Barabara ya Pawaga
Postal Address: P.O.Box 858, 51108 Gangilonga, Iringa, Tanzania
Telephone: +255 262 702 715
Mobile:
Email: ras@iringa.go.tz
Copyright ©2024 Iringa Regional Secretariat. All rights reserved.